'Nikiwa mdogo niliwahi gonjeka sana mpaka nikafariki' - Stevo asimulia maisha ya utotoni

Akiwajibu wale wanaomnyanyapaa kutokana na maumbile yake wakitania sura yake, Stevo alisema, “msihukumu mtu, Mungu ndiye anajua kwa ajili yake aliumba Stevo, mpaka akampa neema.”

Muhtasari

• Msanii huyo alifunguka kwamba alipofanya mtihani wa darasa la nane, hakuweza kuendelea na masomo yake kwani hakufaulu vizuri kuingia shule ya sekondari.

Stevo Simple Boy
Stevo Simple Boy
Image: Facebook

Kwa mara ya kwanza, msanii Stevo Simple Boy amefunguka kuhusu maisha yake ya utotoni – jambo ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza bila kupata jawabu.

Stevo alifunguka kwamba akiwa mdogo, hakupata maisha ya kufurahiwa na kila mtoto, akisema kwamba utotoni mwake, alitawaliwa na ugonjwa hadi mamake mzazi kwa kipindi Fulani akatamauka na kupona kwake.

Katika kile ambacho ni cha kushangaza na ambacho kimewaacha mashabiki wake na maswali mengi, msanii huyo alisema kwamba kwa wakati mmoja aligonjeka hadi kufa lakini akafufuka baadae.

Ilikuwaje?

“Mimi nikiwa mtoto mdogo, nilikuwa niegonjeka sana sana hadi nikafariki. Hadi nikafariki kusema kweli. Ila tu kupitia neema zake Mungu, Mungu akanirejeshea uhai tena. Mamangu mzazi alikuwa amenipeleka hospitali akatamauka akasema huyu ameshaenda. Nilidungwa sindano na kupewa dawa lakini hazikuwa zinafanya kazi, lakini kupitia wokovu wa Mungu, nikafufuka,” Stevo alielezea.

Msanii huyo alifunguka kwamba alipofanya mtihani wa darasa la nane, hakuweza kuendelea na masomo yake kwani hakufaulu vizuri kuingia shule ya sekondari.

“Nilikulia Oyugis nikasoma kutoka chekechea hadi darasa la saba, kutoka hapo nikaja Nairobi Kibera nikafanya darasa la nane lakini sikufaulu. Usanii nilianzia Oyugis lakini Nairobi nilikuja kutafuta ujuzi Zaidi,” alieleza Stevo.

Akiwajibu wale wanaomnyanyapaa kutokana na maumbile yake wakitania sura yake, Stevo alisema, “msihukumu mtu, Mungu ndiye anajua kwa ajili yake aliumba Stevo, mpaka akampa neema.”