Eudoxie Yao apongeza Ivory Coast kwa kujikung'uta mavumbi na kufika robo fainali Afcon

Timu ya Ivory Coast ilianza safari yao ya mashindano ya AFCON kama mwenyeji kwa kusuasua katika kundi lao na kutitigwa kibano cha mabao 4-0 na Equatorial Guinea.

Muhtasari

• Timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya 3 kwenye kundi lao lakini ikafuzu kwa ubora wa mabao katika hatua ya 16 bora.

Eudoxie Yao
Eudoxie Yao
Image: Facebook

Mwanasosholaiti kutoka Ivory Coast, Eudoxie Yao amemimina sifa kochokocho kwa timu ya taifa hilo mwenyeji wa mashindano ya AFCON kwa kujisatiti hadi kutinga robo fainali.

Yao ambaye amekuwa akifuatilia kipute hicho ambacho kiko nyumbani kwao aliwapongeza vijana wa The Elephants of Africa kwa kujizoa kutoka kwa mavumbi ya rekodi mbaya katika hatua ya makundi hadi kutinga robo fainali.

“Hongera Ivory Coast 🇨🇮 kwa ushindi huu mzuri. Senegal 🇸🇳 haikustahili ninajivunia nyinyi 💋💋 wHuko Yamoussoukro hivi sasa alikuwa wamekatisha huduma za mtandao...” aliandika.

Timu ya Ivory Coast ilianza safari yao ya mashindano ya AFCON kama mwenyeji kwa kusuasua katika kundi lao na kutitigwa kibano cha mabao 4-0 na Equatorial Guinea katika mechi ya mwisho ya makundi.

Timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya 3 kwenye kundi lao lakini ikafuzu kwa ubora wa mabao katika hatua ya 16 bora.

Ikiwa na matumaini finyu ya kuendeleza safari yao kwenye kombe hilo na kama mwenyeji, Ivory Coast walikuwa na nafasi finyu baada ya kubaini kwamba waliwekwa kucheza dhidi ya bingwa mtetezi, Senegal katika hatua ya mwondoano.

Lakini kama vile bahati ilisimama upande wao, juzi waliwaondoa Senegal katika kipute hicho kwa kuwashinda katika matuta ya penati baada ya sare ya 1-1 katika muda wa dakika 90 na 30 za nyongeza.

Sasa Ivory Coast watakuwa wanakipiga dhidi ya Mali katika robo fainali.