Georgina Njenga afunguka kuhusu mpango wa kutafuta mtoto wa pili

“Sasa hivi nahisi niko sawa kwa hiyo mashabiki wangu subirini, nitakuwa naachia maudhui baada ya maudhui kwa mpigo. Labda hata tunaweza anza kuleta co-parenting content,” aliongeza.

Muhtasari

• Kuhusu kurejea katika kukuza maudhui baada ya kupotea mitandaoni kwa muda, Georgina Njenga alisema kwamba mashabiki wake wakae mkao.

Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Mkuza maudhui wa TikTok na YouTube, Georgina Njenga ameweka wazi kuhusu mpango wake wa kupata mtoto wa pili.

Akizungumza na mwanablogu Nicholas Kioko, Njenga alisema kwamba kwa sasa hana mpango wowote kuhusu kutafuta mtoto mwingine na kufichua kwamba kilichopo katika fikira zake na kurejelea katika kukuza maudhui muda wote.

 Mrembo huyo mama wa mtoto mmoja alisema kwamba ana uhakika wa asilimia mia fil mia kwamba hatoweza tena kupata mtoto mwingine katika maisha yake, kwani ukurasa wa uzazi ndio hivyo ameshaufunga na bintiye Astra kama mtoto wa pekee.

“Kuhusu mtoto wa pili, hapana. Hapana kabisa, niko sawa. Kabisa nimeshaufunga ukurasa huo 100%,” alisema.

Kuhusu kurejea katika kukuza maudhui baada ya kupotea mitandaoni kwa muda, Georgina Njenga alisema kwamba mashabiki wake wakae mkao wa kula akidokeza kwamba huenda wakaungana na babydaddy wake kuanza kufanya video za kutoa mafunzo jinsi ya kushirikiana kulea mtoto baada ya kutengana na penzi kuvunjika.

“Sasa hivi nahisi niko sawa kwa hiyo mashabiki wangu subirini, nitakuwa naachia maudhui baada ya maudhui kwa mpigo. Labda hata tunaweza anza kuleta co-parenting content,” aliongeza.

Mrembo huyo mama wa mtoto mmoja alisema kwamba awali alikuwa anatatizika kuhusu suala la kumleta mwanawe Astra katika maisha ya mitandao ya kijamii lakini kwa sasa ameshazoea jinsi utandawazi unavyoenda.