Fahamu sababu ya KRG kulazimika kufunga klabu yake ya starehe ya Casa Vera

“Kwa sababu ya hali ilivyo, mnaona biashara ni kama hakuna kitu kinaendelea hapa. Leo ndio tarehe rasmi ya kufungwa kwa Casa Vera" KRG alitangaza.

Muhtasari

• "Na hii najua ni habari mbaya kwa watu ambao wanafanya kazi hapa, wale ambao wanapenda kupata burudani hapa na pia kwa umma na mashabiki wa KRG" aliongeza.

Msanii na mmiliki wa klabu ya Casa Vera
KRG the Don// Msanii na mmiliki wa klabu ya Casa Vera
Image: Facebook

Msanii KRG the Don ametangaza kufungwa kwa baa inayohusishwa kuwa chini ya umiliki wake katika mtaa wa kifahari wa Kilimani jijini Nairobi, Casa Vera Lounge.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni jioni ya Alhamisi, Bughaa kama anavyojiita alisema kwamba kwa muda sasa hakuna biashara ambayo imekuwa ikifanyika vizuri na hivyo hiyo ndio ilikuwa siku ya mwisho ya kufungwa kwa klabu hicho cha starehe.

“Kwa sababu ya hali ilivyo, mnaona biashara ni kama hakuna kitu kinaendelea hapa. Leo ndio tarehe rasmi ya kufungwa kwa Casa Vera. Na hii najua ni habari mbaya kwa watu ambao wanafanya kazi hapa, wale ambao wanapenda kupata burudani hapa na pia kwa umma na mashabiki wa KRG ambao wamekuja kunisapoti kwa muda mrefu, kwa hiyo kutoka sasa hatutakuwa tunafanya kazi mpaka pale tutakapotoa taarifa baadae,” KRG alisema kwa kusikitika.

Hata hivyo, msanii huyo aliweka wazi kwamba Casa Vera haitafungwa milele bali itakuja kufunguliwa siku moja baada ya marekebisho ya kile alichokitaja kuwa ni malalamiko kutoka kwa majirani kuhusu kelele za muziki kutoka kwa sehemu hiyo ya starehe.

“Hatufungi permanently, bali tunafunga kwa sababu tunataka kuboresha huduma zetu, najua inauma hata mimi inaniuma kwa sababu mnavyojua mimi ni mtu napenda kufanya kazi, pesa na maisha mazuri. Imetubidi tufunge kwa sababu tunataka kuboresha baadhi ya vitu ili tufikie viwango vya watu ambao tunaburudisha hapa na pia serikali, yaani tuwe vizuri pande zote ili biashara iwe nzuri kwa kila mtu,” aliongeza.

“Tumekuwa tukipata malalamiko kutoka kwa majirani wa eneo hili la Kilimani wanasema tunawapigia kelele usiku, na ndio maana tumeamua kufanya hivi,” aliongeza.