Alikiba: Nimemtoa Diamond namba 1 akiwa na Jay Melody na Mr Blue, sio peke yake!

Alikiba aliwakumbusha mashabiki kwamba hakumtoa tu Diamond peke yake bali alimtoa pamoja na wasanii wengine Jay Melody na Mr Blue aliowashirikisha kwenye 'Mapoz'

Muhtasari

• Alikiba alifika kwenye ukurasa wa blogu moja iliyoripoti taarifa hizo na kusema kwamba “Nandy na Alikiba wamtoa Diamond namba moja, muda huu ‘Dah’ ndio namba moja sasa.”

Msanii anayetajwa kama muimbaji bora wa Bongo Fleva, Alikiba ameotesha upya mchezo wake wa kujibizana kwa kauli tata za ucheshi na mpinzani wake wa muda mrefu Diamond Platnumz.

Baada ya wimbo wake alioshirikishwa na Nandy ‘Dah!’ kuupiku wimbo wa Diamond aliowashirikisha wakali wa muziki Jay Melody na Mr Blue ‘Mapoz’ kwenye nambari moja katika mtandao wa YouTube kwenye trending, Alikiba amepata mwamko mpya wa kuonesha jinsi alivyo mbabe kuliko Diamond.

Media mbali mbali ziliripoti juzi kati kwamba Alikiba na Nandy walifanikiwa kumng’oa Diamond kwenye nambari moja ambapo alikuwa amejidai kwa muda mrefu kuwa hakuna msanii mwenye umwezo wa kumtoa nambari moja pindi wimbo wake unapotua kileleni.

Alikiba alifika kwenye ukurasa wa blogu moja iliyoripoti taarifa hizo na kusema kwamba “Nandy na Alikiba wamtoa Diamond namba moja, muda huu ‘Dah’ ndio namba moja sasa.”

Hata hivyo, Alikiba alionekana kutofurahishwa na kauli hiyo na kumkumbusha mwanablogu huyo kwamba si Diamond pekee bali ni pamoja na wasanii wengine.

Alikiba aliandika;

“Akiwa na Jay Melody na Mr Blue, sio peke yake.”

Juzi akitupa kijembe kwa Diamond, Alikiba alitumia mstari wa wimbo wa Mapoz kwamba ‘matikiti yanadondoka yakidondokeana’ na kusema kwamba yeye na Nandy wameyaangusha matikiti ya watu kutoka namba moja kwenye trending.