Watu hawangenijua mimi bila mchango mkubwa wa Rose Muhando - Annastacia Mukabwa

"Yeye [Rose Muhando] ndiye Mungu alimpatia ufunuo na kuona kilicho ndani yangu, akanishika mkono na yeye ndiye alinipeleka studio na akalipa pesa zake na leo hii mnamsikia Annastacia,” alisema.

Muhtasari

• Msanii huyo aliambia mwanablogu Trudy Kitui kwamba kolabo ya ‘Kiatu Kivue’ ya karibia miaka 15 iliyopita ndiyo iliyomfanya Annastacia Mukabwa ambaye anajulikana sasa hivi.

Annastacia Mukabwa na Rose Muhando
Annastacia Mukabwa na Rose Muhando
Image: Facebook

Mwinjilisti Annastacia Mukabwa kwa mara ya kwanza amezungumzia uhusiano wake na malkia wa injili kutoka Tanzania Rose Muhando.

Mukabwa amefunguka kwamba mpaka leo hii anamheshimu Rose Muhando Zaidi ya kuwa rafiki yake, yeye anamuona kama mbeba hatima yake ambaye alifanya mchango mkubwa mpaka Mukabwa kujulikana.

Msanii huyo aliambia mwanablogu Trudy Kitui kwamba kolabo ya ‘Kiatu Kivue’ ya karibia miaka 15 iliyopita ndiyo iliyomfanya Annastacia Mukabwa ambaye anajulikana sasa hivi.

“Rose Muhando si tu kwamba ni rafiki wangu, yeye ni kielelezo changu. Unaposikia Annastacia amesimama anamtumikia Mungu, yeye [Rose Muhando] ndiye Mungu alimpatia ufunuo na kuona kilicho ndani yangu, akanishika mkono na yeye ndiye alinipeleka studio na akalipa pesa zake na leo hii mnamsikia Annastacia,” alisema.

“Rose Muhando ndiye mwanamke nyuma ya mafanikio yangu katika fani ya muziki,” aliongeza.

Mukabwa alisema kwamba kupitia kwa moyo huo wa kushikwa mkono na kusaidiwa, naye pia amejibidiisha kufanya hivyo lakini akaweka wazi kwamba hatoweza kuimba na kila mtu katika dunia hii bali atafanya kuchagua yule ambaye anahisi ana kitu cha kweli ndani mwake.

“Kuna wale ambao pia wamenitafuta na wakaomba niimbe na wao. Sitaimba na kila mmoja katika dunia hii lakini nitaimba na wale ambao nitajisikia kuna muunganiko kati yetu, kwa sababu shetani pia naye ana njia yake ya kupackage watu na kuwaleta. Kwa hiyo pia nahitaji kuwa makini nijue kwamba huyu ni mtuminishi wa Mungu, ako na kitu na hana mtu wa kumshika mkono,” alisema.