Eric Omondi kuwa mpatanishi wa amani baina ya Mungai Eve na Trevor

"Kama hawatafanya kazi pamoja basi warudiane au kuwa marafiki, sio eti nalazimisha lakini ni kitu mimi naona nitahakikisha kimefanyika,” alisema Omondi.

Muhtasari

• “Najua kadhia ni kwamba watu wakisha achana basi wanakuwa maadui, lakini kwa Trevor na Eve ni sharti wafanye kazi." alisema.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: Facebook

Mchekeshaji ambaye ni mwanaharakati Eric Omondi ametangaza kuanzisha mchakato wa kuwapatanisha Mungai Eve na aliyekuwa mpenzi wake Director Trevor.

Omondi alifichua haya wakati wa mahojiano na Trudy Kitui ambapo alisema kwamba yeye ana mchango mkubwa sana katika makuzi ya chaneli ya Eve Mungai na mapenzi yake na Trevor tangu wakiwa malimbukeni katika tasnia ya ukuzaji wa habari za mitandaoni.

Akijiita kama baba katika maisha ya wawili hao, Omondi alisema kwamba ana kila haki ya kuhakikisha ana usemi katika uhusiano wa wawili hao ambao unadaiwa kusambaratika wiki kadhaa zilizopita mpaka hivi Juzi Trevor alipoamua kumfuta Mungai kazi na kuibadilisha chaneli ya YouTube jina.

Mwanaharakati huyo alisema kwamba anamsubiria Mungai Eve kurejea nchini kutoka Zanzibar ili kuandaa kikao cha pamoja na kuhakikisha kwamba wanapatana, hata kama hawatarudiana kimapenzi basi atahakikisha mwafaka wa kufanya kazi pamoja umepatikana.

“Katika suala la Eve na Trevor, nafikiri nina haki ya kuzungumza. Eve na Trevor nataka mimi kama Eric Omondi, kwa sababu nimewakuza, nataka kuzungumza na wote. Nataka kuwanunulia chakula kwa lazima,” alisema.

“Najua kadhia ni kwamba watu wakisha achana basi wanakuwa maadui, lakini kwa Trevor na Eve ni sharti wafanye kazi. Kama hawatafanya kazi pamoja basi warudiane au kuwa marafiki, sio eti nalazimisha lakini ni kitu mimi naona nitahakikisha kimefanyika,” alisema Omondi.

Alisema kwamba atawakutanisha na kuwanunulia Nyama Choma na kuwakumbusha pahali walitoka wakiwa pamoja, huku akisema kwamba hata hivyo haitakuwa kama anawalazimisha warudiane, bali anachokitaka ni wasichukiane.

Ni hivi majuzi Trevor aliulizwa na mashabiki wake na kusema kwamba tayari ameshabadilisha jina la akaunti ya Facebook na chaneli ya YouTube kutoka kwa Mungai Eve hadi kwa Kenya Online Media.

Trevor aliweka wazi kwamba huduma za Mungai Eve zimeshafika mwisho na hazihitajiki tena katika chaneli hiyo, hivyo kumtema.