Binti wa kwanza wa taifa, Charlene Ruto amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya video kuibuka kutoka kwa mkutano mkubwa wa maombi ugani Nyayo ulioongozwa na mwinjilisti kutoka Marekani Benny Hinn akitoa ombi la Kutaka ndoa.
Katika video hiyo ambayo imeenezwa katika mtandao wa X, binti Ruto alionekana akiwa amepanga foleni katika wale ambao walikuwa na maombi maalum kutoka kwa mtumishi wa Bwana.
Benny Hinn, mwinjilisti Mmarekani mwenye asili ya Israeli aliwasili nchini wikendi iliyopita na kuongoza mkutano mkubwa wa maombi katika uwanja wa Nyayo.
Charlene Ruto alionekana akimnong’onezea masikioni Benny Hinn kabla ya kutamka kwenye kipaza sauti kwamba ‘hio ndilo unataka niombee?’ kisha akaenda mbele na kuombea takwa la Binti wa taifa.
Mtu wa Mungu alianza kuomba:
"Mpe mume ambaye atatimiza wito huo pamoja naye. Bwana, mpeleke kijana huyo njia yake ambayo itakuwa nguvu kwake, msaada mkubwa kwake. Hawezi kufanya hivi peke yake Bwana, anaenda kwenye uwanja wa vita ili kushinda roho, kuchukua roho kutoka kwa adui. Anahitaji mume upesi, Bwana. Mpeleke njia yake. Mwache awe vile hasa anavyotaka. Kila kitu anachotaka kuhusu mumewe mpe, Bwana."
Mhubiri alimwombea, na akaanguka wakati wa upako. Alikaa chini kwa dakika chache kabla ya kusimama.
Baada ya maombi, Benny alimshika Charlene mkono na kusema maneno fulani, akiomba uwanja mzima, kutia ndani wazazi wake, kurudia baada yake.