Shakib Cham akasirishwa baada ya kuulizwa swali kuhusu urafiki wake na Diamond (video)

Shakib bado roho yake ni nyeusi kwa Diamond haswa baada ya kuonekana kwenye video akiwa ameshikana mkono kimahaba na mpenzi wake Zari.

Muhtasari

• Zari hata hivyo alijutia kutomuambia Shakib kuhusu video hiyo kabla.

• Kwa maneno yake, Zari alisema kwamba uhusiano wake na Shakib umeingia doa na wamekuwa wakizozana tangu Novemba mwaka jana.

Diamond amesifia mahaba mazito ya Shakib kwa Zari
Image: HISANI

Shakib Cham Lutaaya, mume wa Zari hataki kabisa kuzungumza chochote kuhusu msanii Diamond Platnumz – haswa baada ya video kuibuka akiwa ameshikana mikono na Zari.

Katika mahojiano na vyombo vya habari nchini Uganda saa chache baada ya Zari kukiri kuwepo kwa mpasuko katika penzi lao, Lutaaya, mume wa Zari Hassan (ambaye ana watoto wawili na Platnmuz), aliulizwa na mwandishi: "Tulikuona na Diamond wakati fulani huko nyuma, uhusiano wako ukoje?"

Katika kile kilichoonekana kama hataki kabisa kulisikia jina la Diamond, Shakib alijibu: "Nadhani hiyo ni mada ya siku nyingine; tumemaliza kwa leo?"

Mwandishi alisisitiza zaidi: "Lakini kuna uhusiano?"

Shakib alisisitiza: "Mada ya siku nyingine."

Hii inakuja miezi michache tu baada ya Shakib kuonekana wakifurahia wakati mzuri na Diamond kwenye kochi moja huku nyuma yao Zari akiwa amesimama pia na Zuchu – anayetajwa kuwa mpenzi mpya wa Diamond.

Baadae Zari alikuja kutoa mwanga Zaidi kuhusu kikao hicho, akisema kwamba baba watoto wake – Diamond – alikuwa anatamani kukutana na Shakib ili kumjua ni mtu wa aina gani ambaye anatumia muda mwingi na wanawe, Tiffah na Nillan.

Hata hivyo, video ya mwishoni mwa juma ikiwaonyesha Zari na Diamond wakiwa wameshikana kimahaba huenda ndicho kichocheo kikubwa cha Shakib kupandwa na mori na kuondoka nyumbani, kwa mujibu wa Zari.

Zari hata hivyo alijutia kutomuambia Shakib kuhusu video hiyo kabla.

Kwa maneno yake, Zari alisema kwamba uhusiano wake na Shakib umeingia doa na wamekuwa wakizozana tangu Novemba mwaka jana.

Alisema kwamba video hiyo yake ya Diamond haikuwa na kitu chochote kuhusu mapenzi bali ilikuwa ni tangazo la kibiashara lakini alijuta kutomuelezea Shakib kwa wakati ufaao.