Esma asimulia jinsi Diamond alighairi kuoa baada ya familia kumtafutia mke, kulipa mahari

“Kulikuwa kuna mwanamke mmoja anaitwa Sofia, alipelekewa mpaka mahari kwao. Ilikuwa bado siku sisi twende tujitambulishe kwake rasmi kwenye uchumba kama familia..."

Muhtasari

• "Tulijaribu kumlazimisha aoe lakini tukaona muda wake mwenyewe haujafika,” Esma alisema.

Diamond na dadake, Esma
Diamond na dadake, Esma
Image: Screengrab

Siku chache baada ya Esma Platnumz kufunga harusi na mume mpya, mfanyibiashara Jembe One, amefunguka makubwa na ya ndani kutoka kwa familia yake kuhusu kaka yake, Diamond Platnumz kushindwa kuoa mpaka sasa.

Esma na mumewe walitokea kwenye kipindi cha Masham Sham kwenye Wasafi FM ambapo alifichua kwamba wao kama familia wamejaribu juhudi zote kumshawishi Diamond kutulia katika ndoa lakini yote ikawa kazi bure.

Mjasiriamali huyo wa duka la vitenge na dera alifunguka kwamba kuna wakati wao kama familia waliketi chini na kuafikia wazo la kumtafutia Diamond mke kwa nguvu.

Alisema kwamba Diamond aliridhia japo shingo upande hadi wakalipa mahari na Diamond mwenyewe kushonesha vazi la harusi nchini Uturuki lakini siku ya ndovu kumla mwanawe, msanii huyo alibadili fikira zake na kusema hakuwa tayari kuoa.

“Diamond tushaongea na yeye sana, si unajua kila jambo mwenyezi Mungu ndiye analipitisha. Tunaweza tukamlazimisha aoe halafu hajataka kesho keshokutwa mtoto wa wenyewe amuache?...Tulijaribu kumlazimisha aoe lakini tukaona muda wake mwenyewe haujafika,” Esma alisema.

Hata hivyo, Esma hakubainisha iwapo tukio hilo lilitokea kabla ya uhusiano wake na Zari na Tanasha au baada ya kuachana na wawili hao walioonekana kupendana na kuwa katika penzi zito.

Alifichua hadi jina la mwanamke mwenyewe ambaye familia ilimtolea mahari lakini mwisho wa siku Diamond akatibua shughuli.

“Kulikuwa kuna mwanamke mmoja anaitwa Sofia, alipelekewa mpaka mahari kwao. Ilikuwa bado siku sisi twende tujitambulishe kwake rasmi kwenye uchumba kama familia. Na yeye mwenyewe Diamond alikuwa ameshashona nguo za sare Uturuki na kuandaa kila kitu na mwanamke alikuwa ameshafika mpaka hapa. Lakini ilipofika karibu Diamond akaja akajifikiria nahisi siko tayari, alimfuata yule mwanadada nimekaa nimefikiria lakini nimeona siko tayari, nahisi muda wangu bado hujafika,” Esma alifichua.

Kutibuka kwa shughuli hiyo nyakati za lala salama kulimfanya mamake, Mama Dangote kumtishia kwa mikwara kibao lakini Diamond alishikilia msimamo wake kwamba hayuko tayari kuingia katika ndoa.

“Mama alimsukuma mpaka akafika mahali akamtishia kama mimi sio mama yako… lakini alikaa na mama akasema hawezi kumchukua mtoto wa watu na baadae akaja kumtesa na hivyo familia ilimuelewa,” Esma aliweka wazi.