Andrew Kibe afichua kiasi cha pesa chaneli 6 YouTube zilikuwa zinamuingizia kila mwezi

Hata ivyo, baada ya chaneli hizo zote kufungwa, Kibe alirejea nchini Kenya na sasa anaamini kwamba kulikuwa na mkono wa baadhi ya watu wenye wivu ambao walipelekea kufungwa kwa sehemu ya riziki yake.

Muhtasari

• Katika mahojiano na Mungai Eve, Kibe alifichua kwamba alikuwa na chaneli 6 lakini mbili kati ya hizo ndio bado hazikuwa zimeanza kumuingizia hela.

Andrew Kibe
Andrew Kibe
Image: screengrab,

Mwanablogu Andrew Kibe ambaye amerudi nchini Kenya baada ya chaneli zake za YouTube kufungwa akiwa Marekani amefichua kiasi cha hela alizokuwa anakusanya kutokana na maudhui yake kwenye mtandao huo wa video.

Katika mahojiano na Mungai Eve, Kibe alifichua kwamba alikuwa na chaneli 6 lakini mbili kati ya hizo ndio bado hazikuwa zimeanza kumuingizia hela kabla ya kufungwa ghafla.

Mkuza maudhui huyo alisema kwamba katika chaneli ambazo zilikuwa zinamuingizia hela, kila moja ilikuwa inauingizia takribani dola elfu 10 – sawa na shilingi milioni 1.5 pesa za Kenya kila mwezi.

Hata hivyo, siku moja aliamka asubuhi na kupata kwamba chaneli zake zote sita zimezama bila kutahadharishwa kabla.

Kibe ambaye alikuja kuanzisha jukwaa lake binafsi hata hivyo anaamini kwamba kuna baadhi ya wanablogu wenzake kutoka Kenya ambao walikuwa wanaonea wivu ufanisi wake, ambao ndio waliungana na kuhakikisha wanamripoti kwa mamlaka za YouTube ili kufungiwa.

“Walinifungia chaneli zote 6, ilikuwa ni kitu Fulani kibaya ambacho mtu Fulani alifanya. Na nafikiri wewe na wenzako ndio mlinifanyia hivyo. Mliungana pamoja na mkasema kwamba mgeenda kunishtaki. Si mtu mmoja, naamini ni watu wengi ambao walikuja pamoja baada ya kuona wivu kwa kile nilichokuwa nakipata kutoka YouTube,” Kibe alisema.

“Nilikuwa natengeneza pesa nyingi sana. Chaneli moja ilikuwa inanipa angalau dola elfu 10 kila mwezi. Kitu hakiwezi tokea tu chenyewe, mimi naamini kuna watu Fulani ambao waliona wivu na kwenda kuniripoti kwa YouTube. Chaneli zangu zote 6 zilikunywa maji,” aliongeza.

Kibe alisisitiza kwamba sio mambo ya hakimiliki ambayo yalifanya chaneli zake kunywa maji bali ni watu ambao waliona wivu kuhusu mafanikio yake.