Ezekiel Mutua ajibu kauli ya Nonini ya ‘Heshimu wasanii, wewe ni mfanyikazi wako’

“Hii ilimgeukia, kwa kweli! Ni sawa na mchezaji kumwambia kocha "Tuheshimu. Sisi ni mwajiri wako." Bila shaka kocha hachezi. Lakini anasimamia na kuweka nidhamu katika timu." Mutua alisema.

Muhtasari

• Awali akizungumza kwenye runinga ya Citizen, Nonini alimtaka Mutua kuwaheshimu wasanii akisema kwamba bila wao, yeye asingekuwa na kazi katika ofisi ya MCSK.

Mutua na Nonini
Mutua na Nonini
Image: Facebook

Mzozo baina ya chama kinachosimamia mirahaba na hakimiliki za wasanii nchini MCSK na wasanii wenyewe unazidi kutokota haswa, baina ya bosi wa chama hicho Ezekiel Mutua na msanii mkongwe Hubert Nakitare, maarufu Nonini.

Juzi-kati, Nonini alimtaka Ezekiel Mutua kuwapa wasanii heshima yao kwa kile alichokitaja kuwa wasanii ndio wamemuandika yeye kazi.

Hata hivyo, Mutua kupitia ukurasa wake wa Facebook asubuhi ya Jumanne, alimjibu Nonini kwa kauli hiyo akisema kwamba ni sawa na wachezaji kuanza kumfokea kocha wao wakitaka heshima kwa nguvu kutoka kwake kisa wao ndio wanafanya analipwa.

Mutua aliendelea kwa kuelezea umuhimu wa nidhamu katika Nyanja yoyote, akisema kwamba hata kama kocha hachezi, lakini lazima awepo ili kuhakikisha nidhamu hiyo inapatikana kutoka kwa wachezaji – akijirejelea kama kocha na wasanii kama wachezaji.

“Hii ilimgeukia, kwa kweli! Ni sawa na mchezaji kumwambia kocha "Tuheshimu. Sisi ni mwajiri wako." Bila shaka kocha hachezi. Lakini anasimamia na kuweka nidhamu katika timu. Wasanii wakitaka kuheshimiwa ni lazima wafuate sheria na waunde maudhui ambayo yanakuza utamaduni na maadili ya Kenya,” Mutua alimjibu.

Mkurugenzi huyo wa MCSK alipinga vikali kuheshimiwa kwa wasanii ambao wanapotosha jamii kwa maudhui yenye utata, kama yale ya msanii anayecheza densi akiwa na nepi kwa jina la injili.

Mutua alitetea hatua ya wasanii Embarambamba na William Getumbe kuwajibishwa na KFCB kwani hakuna sekta inayoweza kuendelea na kudumu pasipo na nidhamu pamoja na muongozo Fulani wa kufuatwa.

“Hakuna anayeweza kuheshimu kichaa cha watu kucheza uchi na kuvaa nepi kama watoto wadogo. Hakuna tasnia inayoweza kuendeleza bila nidhamu. Ili wasanii waheshimiwe lazima kuwe na kanuni za maadili. Lazima wawe na viwango vya kitaaluma. Watumie vipaji vyao kujenga na sio kuharibu jamii. Na lazima waiheshimu Serikali na uongozi wao!” Mutua alimaliza.

Awali akizungumza kwenye runinga ya Citizen, Nonini alimtaka Mutua kuwaheshimu wasanii akisema kwamba bila wao, yeye asingekuwa na kazi katika ofisi ya MCSK.

"Kama huwezi kufuata agizo la serikali unafanya nini? Yeye ni mwajiriwa wa wasanii lazima awaheshimu. Tangu lini ukaona mfanyakazi anagombana na wakubwa wake?" Nonini alifoka.

Hii si mara ya kwanza kwa Nonini kuhoji MCSK kuhusu ukusanyaji na usambazaji wake usio wa haki katika tasnia ya muziki nchini Kenya.