Babu Owino atimiza ahadi yake ya kufanya kolabo na Stevo Simple Boy (video)

“Ni wewe Baba umenifanya ning’are, siku zote niko na wewe, siwezi bila wewe. Wacha uabudiwe na tena usifiwe. Kwako baba Baraka tele, furaha tele, umenilinda, nakuita Yahwe" Stevo anaimba.

Muhtasari

• Kolabo hiyo ambayo ilipakiwa kwenye chaneli ya YouTube ya Stevo Simple Boy Jumanne alasiri inakwenda kwa jina Neno.

Babu Owino na Stevo Simple Boy
Babu Owino na Stevo Simple Boy
Image: Facebook

Wasemavy ahadi ni deni, na dawa ya deni ni kulipa!

Hatimaye mwanasiasa Babu Owino ametimiza ahadi yake ya kufanya kolabo ya msanii Stevo Simple Boy.

Kolabo hiyo ambayo ilipakiwa kwenye chaneli ya YouTube ya Stevo Simple Boy Jumanne alasiri inakwenda kwa jina Neno.

Kwenye ‘Neno’ Stevo Simple Boy pamoja na meneja wake Chingiboy Mstado walimshirikisha Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki kwenye video wakiimba na kudensi kwenye ngoma hiyo ya injili.

“Ni wewe Baba umenifanya ning’are, siku zote niko na wewe, siwezi bila wewe. Wacha uabudiwe na tena usifiwe. Kwako baba Baraka tele, furaha tele, umenilinda, nakuita Yahwe, wacha uinuliwe hadi milele. Ndio maana yake napiga vigelegele hata na shangwe,” Stevo Simple Boy anaimba kwenye vesi yake.

Licha ya kutotamka hata neno moja kwenye wimbo huo, Mbunge Owino alionekana kwenye video na huo ulikuwa mchango mkubwa katika kusaidia kuisukuma video hiyo kwa mashabiki wengi Zaidi.

Babu Owino hakuishia hapo, alikwenda kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kuwataarufu mashabiki wake kwamba hatimaye kolabo yake na Stevo imetokea na kuwataka kuitazama.

Owino mwezi mmoja uliopita alitoa ahadi ya kufanya kolabo na Stevo na kuwataka mashabki wake kuwa ange.

Kipindi hicho, Owino aliandika;

“Nilifanya mkutano mzuri na Stevo Simple Boy. Yuko katika tasnia ya utengenezaji wa Juisi ya Freshi Barida inayozalishwa kwa ladha tofauti. Tukuze Simple Boy."

“Pia tutafanya kazi pamoja katika tasnia ya muziki na kolabo itatoka hivi karibuni,”aliongeza.

Mpaka Makala haya yalivyokuwa yanachapishwa, katika saa 19 pekee, video hiyo ilikuwa imejizolea utazamaji mara elfu 35.

Hii si video ya kwanza ya nyimbo za Sanaa ambayo Babu Owino anaonekana. Itakumbukwa msanii Bahati pia kwa wakati mmoja aliwahi faniiwa kumvuta kwenye video yake ya ‘Adhiambo’ akimshirikisha Prince Indah.