Wakili Danstan Omari na MP Silvanus Osoro wamtetea Embarambamba mbele ya KFCB

"Marufuku ya muda ya kuunda maudhui yameondolewa na sasa yuko huru kujihusisha ndani ya mipaka inayokubalika" Osoro alisema baada ya mkutano na msanii huyo na wawakilishi wa KFCB na MCSK.

Muhtasari

• Osoro pamoja na Omari walimkutanisha Embarambamba na wawakilishi kutoka KFCB pamoja na MCSK.

Embarambamba atetewa mbele ya KFCB
Embarambamba atetewa mbele ya KFCB
Image: Facebok

Ni afueni kwa msanii mwenye utata wa injili kutoka eneo pana la Gusii, Embarambamba baada ya wababe kutoka eneo hilo kuja pamoja na kumpa msaada kukabiliana na maagizo mazito ya KFCB kuhusu video zake.

Baada ya KFCB kumtaka msanii huyo kuzifuta video zake zote zenye utazamaji wa milioni 6.4 kutoka kwenye jukwaa la YouTube, msanii huo alisema adhabu hiyo ni kali na ingemsababishia njaa kubwa kwa sababu familia yake inamtegea kutokana na riziki yake ya kufanya video.

Wakili maarufu kutoka eneo la Gusii Danstan Omari na mbunge wa Mugirango Kusini ambaye pia ndiye kiranja wa wengi kwenye bunge la kitaifa Silvanus Osoro walijitokeza kumsaidia kusuluhisha hilo baina yake na KFCB.

Osoro pamoja na Omari walimkutanisha Embarambamba na wawakilishi kutoka KFCB pamoja na MCSK katika ofisi ya mbunge huyo ili kutafuta mwafaka kuhusu kile alichokiagizwa.

 Baadae, mbunge Osoro kupitia mitandao ya kijamii alithibitisha kufanyika kwa mkutano huo na kufichua kwamba hatimaye walifanikiwa kupata japo suluhu kwa msanii huyo.

Osoro alisema kwamba adhabu ya Embarambamba kufungiwa kutofanya video yoyote yenye utata imeondolewa kwa muda na hivyo anaweza kuendelea na kufanya video lakini zisiwe za kuzua tafrani mitandaoni.

Osoro na Omari waliahidi kuendelea kulitafutia ufumbuzi suala la Embarambamba kutakiwa kufuta video zake zote lakini pia kulipa faini ya Zaidi ya milioni 6, ambazo kwa mujibu wa msanii huyo kupata kiasi hicho cha pesa kwa mkupuo ni mtihani mkubwa.

“EMBARAMAMBA anajitolea kuweka maudhui safi kwenda mbele tunapofuata mkondo tofauti wa kusuluhisha mahitaji ya Ksh.6.2M na KFCB. Marufuku ya muda ya kuunda maudhui yameondolewa na sasa yuko huru kujihusisha ndani ya mipaka inayokubalika. Nimefurahi kuwa mwenyeji wa Mkurugenzi Mtendaji wa MCSK Dkt. Ezekiel Mutua na timu, Ag. Mkurugenzi Mtendaji wa KFCB Bi. Nelly Muluka na timu,Washauri Danstan Omari na Shadrack Wambui na Embarambamba Msanii Wa Kisii mwenyewe katika ofisi yangu ya bunge alasiri ya leo…Sasa Embarambamba fanya kwa umakini kaka!!” Osoro aliandika.

Awali baada ya kupokezwa barua kutoka KFCB kufuatia kikao cha mapema wiki hii, Embarambamba aliomba msamaha hadharani na kusema kwamba adhabu hiyo ni nzito kwake.