Natafuta mume lakini naishia kutongozwa na vijana wadogo tu - Khadija Kopa, mamake Zuchu

Mama huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa Zaidi ya miaka 60 alisema watoto wa siku hizi wengi wanamfuata kabisa na kujimaliza mbele yake jinsi wanavyoshindwa kulala kwa ajili ya kumfikiria yeye.

Muhtasari

• Kopa alisema kwamba mtu ambaye atamkubali ni mwenye umri kuanzia miaka 49 kwenda juu.

Khadija Kopa
Khadija Kopa
Image: Screengrab//Wasafi

Mama yake Zuchu, Khadija Kopa amefichua kwamba tangu atangaze kutafuta mume wa kumsitiri, hajawahi fanikiwa kumpata mwanamume mtu mzima bali anaishia kupata akitongozwa na vijana wadogo tu.

Akizungumza katika Masham Sham ya Wasafi FM, Bi Kopa alifichua kwamba muda mwingi anaishia kupata akitongozwa na vijana wadogo, jambo ambalo yeye hataki kwani yeye ni mtu mzima na anamtafuta mtu mzima mwenzake.

Alisema kwamba jambo linalomfanya kutowakata vijana wadogo wanaomtongoza ni kutokana na kwamba vijana hao hawana mapenzi ya kweli bali wanatafuta urahisi wa kimaisha kwenye mteremko.

“Bado sijapata, wanatokezea lakini sitaki vijana mimi. Mungu hajanijaalia kupata mwanamume mtu mzima sijui kwa nini. Mimi sitaki vijana kabisa. Wengi wamekuja ni vijana vijana, umri mdogo, wanapenda mserereko na umaarufu. Haya mambo siyataki, natafuta mtu mzima,” alisema.

Akiulizwa huwa anawajibuje watoto hao wanapomtongoza, Mamake Zuchu alisema;

“Nawaambia wewe mtoto mdogo kwangu haufai kwangu mimi, nenda kawatafute vijana wenzako. Wengine wananifuata DM wengine wananifuata kabisa ana kwa ana na kuniambia wananipenda lakini nawakataa.”

Mama huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa Zaidi ya miaka 60 alisema watoto wa siku hizi hawaogopi, kwani wengi wanamfuata kabisa na kujimaliza mbele yake jinsi wanavyoshindwa kulala kwa ajili ya kumfikiria yeye.

“Watoto wa siku hizi hawaogopi, wamejivisha mabomu wakalipukie mbele kwa mbele. Wanatafuta maisha tu kwa watu wazima wakati sisi tunatafuta mapenzi,” Bi Kopa alisema.

Kopa alisema kwamba mtu ambaye atamkubali ni mwenye umri kuanzia miaka 49 kwenda juu.