Pasta Ng’ang’a aitaka serikali kumfidia bilioni 200 ili kuwaachia ardhi ya kanisa lake (video)

" Mimi niliuziwa na CBK, hilo shamba lilikuwa la benki nyingine ambayo ilifilisika na wakachukua. Haya mambo ya nimeiba yanatoka wapi?” Nga'ng'a aliuliza.

Muhtasari

• Mchungaji huyo alisema kwamba aliinunua mwaka 2004 kwa shilingi milioni 42 na kama serikali inataka kumhamisha kutoka eneo hio, basi wamlipe fidia ya bilioni 200.

Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Image: Screengrab//Sasa TV

Mchungaji wa kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a ameitaka serikali kumfidia kiasi cha shilingi bilioni 200 ili kuwaachia ardhi ya kanisa lake ambayo imekuwa ikizua utata kwa muda sasa.

Ng’ang’a ambaye alifika kamati inayoshughulikia hakimiliki za shamba akiongozana na wakili wake Silvanus Osoro, aliwakabidhi makaratasi yote yanayoonyesha kuwa yeye ni mmiliki halali kwa ardhi hiyo iliyoko katikati mwa jiji la Nairobi.

Ng’ang’a alisema kwamba kuna baadhi ya watu ndani ya serikali wanaotaka kuipaka serikali tope, akisema kwamba ardhi hiyo aliinunua kutoka kwa benki kuu ya Kenya.

Mchungaji huyo alisema kwamba aliinunua mwaka 2004 kwa shilingi milioni 42 na kama serikali inataka kumhamisha kutoka eneo hio, basi wamlipe fidia ya bilioni 200.

“Hili shamba nilipata kutoka kwa CBK miaka 20 iliyopita, nikakopa pesa kutoka kwa benki nikatoa milioni 42. Mwanzoni walikuwa wanasema milioni 32,” Ng’ang’a alisema.

“Juzi ndio nimeona kwamba wameenda kortini wakidai nilinyakua hilo shamba. Mimi niliuziwa na CBK, hilo shamba lilikuwa la benki nyingine ambayo ilifilisika na wakachukua. Haya mambo ya nimeiba yanatoka wapi?”

“Kuna watu ndani ya serikali ambao wanataka kuhujumu wakitumia serikali. Na wanapiga kanisa, lakini sio hii watapiga kwa sababu niko na kila haki. Milioni 42 kipindi hicho ni pesa nyingi sana, na tukalipa. Na kama mnataka nyinyi kama serikali au yeyote yule, njoo mniambie niwauzie, nataka bilioni 200 kwa njia ya kuongea, kwa sababu nilinunua kwa serikali,” alimaliza.