KRG kununua jeneza, kugharamia mwili wa Brian Chira kuhamishwa kwenda mochwari 'nzuri'

" Nilisikia kijana ni yatima, naona tuhamishe mwili kutoka City Mortuary tuupeleke Montezuma na gharama zote mimi nitalipa ikiwemo ya jeneza,” KRG alisema.

Muhtasari

• Jumamosi alasiri, vyanzo vya habari viliripoti kwamba Chira alifariki dunia baada ya kugongwa na gari nyakati za alfajiri akitoka kuserereka klabuni.

KRG na Brian Chira
KRG na Brian Chira
Image: Maktaba

Siku moja baada ya kifo cha tiktoker Brian Chira ambaye mwili wake ulipelekwa na maafisa wa polisi katika makafani ya City, msanii KRG the Don amejitokeza na kuahidi kutoa msaada kwa familia yake.

KRG akizungumza na SPM Buzz, alisema kwamba amehurumia nyanya wa kijana huyo na anajua fika kwamba hawana uwezo wa kuhamisha mwili wake kwenda katika makafani yenye hadhi kidogo.

KRG alisema kwamba yuko radhi kutoa fedha za kuhamisha maiti hiyo kutoka katika makafani ya City ambayo hurundikwa na miili ya watu waliookotwa kutoka sehemu mbalimbali ambao hawajatambulika na kuupeleka katika makafani ya Montezuma.

KRG pia aliahidi kutoa jeneza zuri kwa ajili ya safari yake ya mwisho, licha ya kukiri kwamba hakuwahi juana moja kwa moja na Chira lakini ameguswa na simulizi kwamba yeye ni yatima ambaye alikuwa analelewa na nyanya tu.

“Mimi sikuwahi mjua kijana huyo moja kwa moja. Nilimuona tu siku moja town akipita mahali nilikuwa lakini nilikuwa bize. Hata sikusalimiana na yeye, lakini kwa sababu ya huruma na heshima za mwisho kwa kijana mdogo ambaye amepoteza maisha yake, na pia nikiwa ninajua kwamba familia hawana uwezo kwa sababu nilisikia kijana ni yatima, naona tuhamishe mwili kutoka City Mortuary tuupeleke Montezuma na gharama zote mimi nitalipa ikiwemo ya jeneza,” KRG alisema.

Jumamosi alasiri, vyanzo vya habari viliripoti kwamba Chira alifariki dunia baada ya kugongwa na gari nyakati za alfajiri akitoka kuserereka klabuni.

Kwa mujibu wa ripoti ya plisi ambayo ilionwa na The Star, mwili wa Chira uliokotwa na maafisa hao majira ya asubuhi eneo la Ndenderu kaunti ya Kiambu na kusafirishwa hadi makafani ya jumla ya City.

Chira alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwani.