Maribe afichua urafiki wake na Itumbi umedumu kwa miaka 20, aahidi kumtafutia mke

Maribe alifichua kwamba yeye na wenzake katika picha za zamani pamoja na Itumbi watahakikisha mwaka huu Itumbi anapata jiko, akiwataka watu kukoma kuwa na dhana kwamba ni yeye atakuwa mke.

Muhtasari

• Maribe alisema kwamba urafiki wao katika kipindi hicho umekumbwa na panda-shuka za kimaisha lakini mwisho wa siku wote wamehakikisha kwamba haufifii.

Dennis Itumbi, Jacque Maribe na Jowie Irungu
Dennis Itumbi, Jacque Maribe na Jowie Irungu
Image: MAKTABA

Rafiki wa karibu wa rais William Ruto, Dennis Itumbi anasherehekea siku yake ya kuzaliwa, na watu mbali mbali wamemtumia jumbe za heri njema.

Mmoja wa watu waliomtakia heri njema ni mwanahabari Jacque Maribe, ambaye kupitia Instagram amemuandikia ujumbe wenye kheri akisema kwamba Itumbi ni mmoja wa marafiki wa kweli ambao ni adimu kupatikana.

Maribe alipakia picha ya pamoja wakiwa na Itumbi miaka ya nyuma na kufichua kwamba urafiki wao haujaanza leo wala jana, bali ni urafiki ambao umefanikiwa kudumu kwa Zaidi ya miongo miwili.

Maribe alisema kwamba urafiki wao katika kipindi hicho umekumbwa na panda-shuka za kimaisha lakini mwisho wa siku wote wamehakikisha kwamba haufifii.

“Heri njema ya siku ya kuzaliwa Dennis Itumbi. Kipindi cha miongo miwili cha urafiki dhabiti kimekuwa ni ushuhuda tosha wa kupanda na kushuka lakini pia na mapenzi sawia,” aliandika.

Maribe pia alimhakikishia Itumbi kwamba kundi la watu waliopiga picha nao kipindi hicho wataungana na kuhakikisha wanamtafutia Itumbi mke.

“Kundi hili unaloliona hapa kwenye hii picha tutaungana kukutafutia mke, kwa hiyo kila mtu achene kudhania kwamba ni mimi mke. Heri njema ya kuzaliwa D.I,” alimaliza.

Dennis itumbi maribe
Dennis itumbi maribe

 Kwa upande wake, Itumbi kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii alisema anasherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kuitoa kwa ajili ya kundi la mchezo wa kuigiza la shule ya wasichana ya Kangaru.

“Ninaweka wakfu siku yangu ya kuzaliwa kwa Klabu ya maigizo katika Kangaru Girls. You guys pulled a good surprise na hata nyinyi mnanifurahisha roho...Mmeanza mwaka wangu kwa kasi sana!! Kwetu sote, wacha tuendelee kuunda kumbukumbu! Huu ni mwaka wa kuunda kumbukumbu mpya na kuandika upya hadithi. Nawapenda wote!” Itumbi alisema.

Itakumbukwa Itumbi amekuwa katika mstari wa mbele kumpa moyo na faraja Maribe wakati wa kesi ambayo alikuwa anatuhumiwa kushirikiana na Jowie katika mauaji ya mfanyibiashara Monica Kimani.

Kesi hiyo ilikamilika wiki chache zilizopita ambapo Maribe aliondolewa mashtaka yote huku Jowie akihukumiwa kifo.