• KRG si mgeni kwa kauli za kujisifia kwa utajiri wake, kila mara akidai kwamba ndiye msanii pekee mwenye utajiri uliovuka kiwango cha bilioni.
Mwishoni mwa wiki jana, msanii KRG the Don alikuwa miongoni mwa wasanii wachache wa Kenya walioalikwa rasmi kuhudhuria uzinduzi wa media ya Alikiba, Crown Media.
Baada ya kurejea nchini, msanii huyo mwenye tambo aliwakejeli Tanzania na wasanii wao wote akisema kwamba yeye ni mkubwa hata kuliko nchi hiyo yote.
Katika mahojiano na SPM Buzz, KRG alisema kwamba aligundua uchumi wa jiji la Nairobi pekee unazidi uchumi wa taifa zima la Tanzania.
Pia alijipiga kifua kwamba ana uwezo mkubwa wa kuinunua nchi hiyo yote pamoja na wasanii wao wote, kuanzia yule mkubwa kabisa hadi yule ambaye anachipukia leo.
“GDP ya Nairobi, pesa inazunguka tu Nairobi pekee, hata Tanzania nchi nzima haiwezi fika. Hiyo ni siri nimewaambia ambayo hamkuwa mnajua. Halafu ucheze na Wakenya wewe? Mimi naweza nunua Tanzania wasanii wao wote kutoka Diamond mpaka yule anatokea leo wakishikanishwa, wote nawanunua na nawaambia ni Bughaa,” KRG alijipiga kifua.
Msanii huyo alizidi kutamba akisema kwamba hata akaamua kulala tu kwa miaka kumi kuanzia sasa, hakuna msanii wa Tanzania anayeweza kufikia utajiri wake.
KRG si mgeni kwa kauli za kujisifia kwa utajiri wake, kila mara akidai kwamba ndiye msanii pekee mwenye utajiri uliovuka kiwango cha bilioni.
Cha kushangaza ni kwamba, licha ya kujidai kw asana, msanii huyo hajawahi jumulishwa katika orodha ya Forbes ya wasanii matajiri Zaidi ukanda wa Afrika Mashariki.
Orodha ya mwaka jana ilimuweka msanii na mwanasiasa kutoka Uganda Bobi Wine kileleni huku Diamond akishika nafasi ya pili.
Wengine waliojumuishwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Jose Chameleone, Akothee, Sauti Sol, Jaguar, Harmonize, Alikiba miongoni mwa wengine bila kuwepo kwa KRG.