KRG afichua kwa nini aliguswa na msiba wa Brian Chira na kutoa msaada wa kuhamisha mwili

“Mtu hajawahi patwa na msiba anadhani ni rahisi. Mtu ambaye amepatwa na msiba atajua ina maana gani kupatiwa hata huo msaada kidogo. Mimi sitaki kupata sifa," KRG alisema.

Muhtasari

• "“Kwa sababu pale City Mortuary kama mnavyojua mambo yake yamechemka, ni mahali ya mambo mengi, hapa ni mahali ya kila kitu ikifanyika ni hapo," KRG alisema.

KRG the DON.
KRG the DON.
Image: Screengrab

Msanii KRG the Don amefichua kwa nini aliguswa na msiba wa TikToker Brian Chira na kufikia hatua ya kutoa msaada wa kuhamisha mwili wake kutoka makafani ya City kwenda katika makafani nyingine.

Akizungumza na SPM Buzz, KRG aliwakosoa wanaomdhihaki kwa kutoa msaada huo, akisema kwamba wengi wa wale wanaosema msaada huo ni mdogo ni wale ambao hawajawahi patwa na msiba.

“Mimi nilirudi kutoka shughuli zangu Tanzania nikapatana ha hizi habari nikasema tu kwa jinsi nilivyomuona yule kijana, ilinigusa. Nikasema tu kwa sababu niliona ni mtu maarufu TikTok, tutoe mwili hapa City tupeleke pale Montezuma ndio hata marafiki zake wakikuja kumuona, inakuwa afadhali kidogo.”

“Kwa sababu pale City Mortuary kama mnavyojua mambo yake yamechemka, ni mahali ya mambo mengi, hapa ni mahali ya kila kitu ikifanyika ni hapo, nikasema acha tupeleke mahali ingine ambayo hata watu wanaweza pata nafasi ya kwenda kumuona vizuri na hata familia itulie kidogo. Nikajitolea kutoa jeneza na ada ya kuhamisha mwili, hayo mengine lazima familia ikae chini kwanza,” KRG alisema.

“Mtu hajawahi patwa na msiba anadhani ni rahisi. Mtu ambaye amepatwa na msiba atajua ina maana gani kupatiwa hata huo msaada kidogo. Mimi sitaki kupata sifa, na chenye mtasema mimi siko katika biashara zenu,” aliongeza.

Mapema wiki hii, KRG alijitolea kufadhili kuhamishwa kwa mwili wa Chira kutoka katika makafani ya City kwenda Montezuma pamoja pia na kununua jeneza.

Chira alifariki wikendi iliyopita baada ya kudaiwa kugongwa na gari nyakati za alfajiri alipokuwa akitoka kwenye tafrija.

Maafisa wa polisi waliuondoa mwili wake eneo la tukio huko Ndenderu na kuupeleka katika makafani ya jumla ya City.