Siri ya ndoa ni urafiki na heshima kwanza, halafu mapenzi yanakuja baadae - Lulu Hassan

“Mimi sipendi kuita Rashid kama bwana yangu, huwa namuita swahiba wangu yaani beshte wangu. Wale wa kuitana ‘mume wangu mume wangu’ katika hiki kizazi, atajiona kama amekuwa mtumwa."

Muhtasari

• "Kwa hiyo yeye ni rafiki yangu kwanza na ananiheshimu na mimi namheshimu, halafu tunapendana,” Lulu alisema.

Rashid Abdalla amtakia kheir ya kuzaliwa mkewe Lulu Hassan.
Rashid Abdalla amtakia kheir ya kuzaliwa mkewe Lulu Hassan.
Image: INSTAGRAM// RASHID ABDALLA

Mwanahabari wa runinga ya Citizen, Lulu Hassan amefichua siri ya ndoa yake kuwa yenye ufanisi mkubwa na mumewe Rashid Abdallah kwa Zaidi ya miaka kumi sasa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa chapa ya Downy, ambapo pia yeye ndiye balozi rasmi, Lulu alisema kwamba siri ya ndoa kuwa imara kwa muda mrefu ni urafiki na heshima kwanza.

Lulu alisema kwamba yeye hamchukulii mumewe Rashid kama mume bali anamchukulia Zaidi kama rafiki na mapenzi pamoja na virutubishi vingine katika ndoa huja baadae.

“Siri ya ndoa ni urafiki na heshima kwanza, hivyo viwili vinakuja kwanza halafu kuna mapenzi na vingine vinakuja baadae. Lakini kwanza awe rafiki yako, mimi huwa naambia kila mtu, huwezi olewa na mtu ambaye si rafiki yako,” Lulu Hassan alipakua siri.

Alifunguka kwamba muda wote yeye na mumewe ambao wanafanya kazi kwenye kampuni moja na kitengo kimoja huwa wanaongozana kutoka na kurudi nyumbani, kwa kipindi cha Zaidi ya miaka 7 ambayo wamekuwa wakifanya kazi pamoja.

“Mimi sipendi kuita Rashid kama bwana yangu, huwa namuita swahiba wangu yaani beshte wangu. Wale wa kuitana ‘mume wangu mume wangu’ inakuwa na changamoto kidogo kwanza hiki kizazi, atajiona kama amekuwa mtumwa. Lakini heri muwe marafiki ndio akikuambia tufanye hivi na hivi mnasaidiana. Kwa hiyo yeye ni rafiki yangu kwanza na ananiheshimu na mimi namheshimu, halafu tunapendana,” Lulu alisema.

“Kitu ambacho watu hawaelewi mara nyingi huwa tunatoka pamoja nyumbani kwenda kazini, na tunarudi pamoja. Miaka yote mpaka sasa hivi tunakuja kazini pamoja na kurudi pamoja, isipokuwa pengine kuna dharura,” aliongeza.