Eric Omondi atangaza kufanya mkutano mkubwa na wahitimu wasio na ajira, Jumanne

"Acha tukutane kesho, Jumanne kuanzia saa tatu asubuhi katika mgahawa wa Bluesprings, barabara ya Thika,” Eric Omondi alisema.

Muhtasari

• “Kama unahitaji kazi, kama wewe ni mjasiriamali, kama una wazo kuja kesho katika mkutano huo, tusichelewe tafadhali, tupatane kwa suluhisho iko kazi,” aliongeza.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: Instagram

Mwanaharakati na mchekeshaji wa zamani Eric Omondi ametangaza kufanya mkutano na wahitimu kutoka vyuo vikuu ambao hawana kazi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Omondi alishiriki video akiwa amevalia gauni la kuhafili na kutoa tangazo hilo kwamba Jumanne kutakuwa na mkutano mkubwa wa wahitimu wasio na kazi jijini Nairobi.

Omondi alifichua kwamba siku chache zilizopita baada ya kutangaza kutumiwa namba za wahitimu wote ambao hawana kazi, alishangazwa na idadi ya namba alizopokea na hivyo amefikia azimio la kuitisha mkutano na wahitimu hao.

“Siku chache zilizopita tuliwaita wahitimu wote wasio na kazi kututafuta, namba zilikuwa nyingi. Sasa tuna jawabu, na hilo jawabu liko mikononi mwetu. Ninatoa wito kwa kila mtu ambaye yuko Nairobi, ambaye ni mhitimu asiye na kazi, tuna suluhisho kwenu, acha tukutane kesho, Jumanne kuanzia saa tatu asubuhi katika mgahawa wa Bluesprings, barabara ya Thika,” Eric Omondi alisema akitoa maelekezo Zaidi kuhusu uliko mgahawa huo.

“Kama unahitaji kazi, kama wewe ni mjasiriamali, kama una wazo kuja kesho katika mkutano huo, tusichelewe tafadhali, tupatane kwa suluhisho iko kazi,” aliongeza.

Omondi amekuwa katika mstari wa mbele akiongoza vuguvugu la #SisiKwaSisi kuwachangia Wakenya wenye mahitaji mabli mbali.

Tangu azindue vuguvugu hilo, Omondi amejitokeza na kunyoosha mkono wa msaada kwa visa mbalimbali, vingi vikiwa ni kusimamia matibabu kwa familia zisizojiweza.

Kuwa kwake tayari kwa kuwaongoza wakenya kutoa msaada kumevutia uvumi mbalimbali, baadhi wakihisi kwamba anatengeneza njia ya kujitoma kwenye siasa katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo, Omondi hajawahi weka wazi kuhusu ni wadhifa upi wa kisiasa atawania lakini akaweka wazi kwamba atajitoma katika jukwaa la siasa akidai kwamba hiyo ndio njia pekee ya kupata nafasi ya kipekee kuwahudumia watu na mahitaji yao.