Kila unayemuona karibu yangu alikuwepo wakati sina kitu, akiwemo mke wangu - Davido

Msanii huyo alisema licha ya kufaulu pakubwa kimuziki, yeye bado ni yule yule kwa marafiki wake wa zamani wala hajabadilika wala kubadilisha marafiki baada ya kutoboa kimuziki.

Muhtasari

• Kulingana na Davido, Chioma amekuwa akimsaidia katika wakati mgumu zaidi na hakuweza kuchagua mwanamke mwingine yeyote kando yake.

• "Ndio ni vizuri, watu hawa wote unaowaona karibu nami walikuwepo wakati sikuwa na kitu .... Nataka aina ya watu wanaoniona kuwa si kitu na sasa wananiona kama kitu".

Staa wa Nigeria, David Adeleke, almaarufu Davido, amezua gumzo mitandaoni kutokana na kauli yake ya hivi majuzi kuhusu mke wake, Chioma Rowland na kila mtu anayeonekana karibu yake.

Davido, ambaye ni mtoto wa mfanyabiashara Bilionea, alikuwa katika onyesho la hivi punde la Ufaransa The Bridge pamoja na nyota wa Real Madrid Aurelien Tchouameni, Cindy Bruna na François-Henry Bennahmias, ambapo alifichua kwamba alikutana na Chioma kabla ya kuwa tajiri.

Kwenye onyesho hilo, mwimbaji huyo wa ‘Unavailable’ kuhusu ndoa yake na kwa nini alichagua kuoana na Chioma, alisema kwamba mrembo huyo alisimama na kuiaminia ndoto yake kipindi ambacho hakuna mtu aliyekuwa akimuaminia kutusua kimuziki.

Kulingana na Davido, Chioma amekuwa akimsaidia katika wakati mgumu zaidi na hakuweza kuchagua mwanamke mwingine yeyote kando yake.

Akiwa kwenye The Bridge, mwimbaji huyo alifichua kuwa alikutana na Chioma, na walianza kuchumbiana kabla ya kuwa na pesa.

Alibainisha kuwa ikiwa hangekutana na Chioma hapo awali, umaarufu na utajiri alionao kwa sasa ungemfanya kuwa mgumu sana kutulia na mwanamke yeyote.

"Nilikutana na mke wangu kabla ya kuwa na pesa na nilikuwa nikijiambia ikiwa sikukutana naye na sasa, nilikuwa peke yangu, haitakuwa sawa," Davido alisema kwenye video hiyo iliyoenezwa mitandaoni.

Kando na mke wake, Davido pia alisema kwamba kila mtu anayemzunguka katika maisha yake ya sasa hivi akiwa tajiri, ni wote ambao walikuwa karibu yake kipindi anahangaika kutoboa kimuziki, wala hajabadilisha marafiki.

"Ndio ni vizuri, watu hawa wote unaowaona karibu nami walikuwepo wakati sikuwa na kitu .... Nataka aina ya watu wanaoniona kuwa si kitu na sasa wananiona kama kitu".

Ikumbukwe kwamba hivi majuzi Chioma alifichua jinsi alivyokutana na Davido kwenye alma-mater, Babcock, Licha ya kukutana mwaka wa 2013, waliendelea kuwa marafiki hadi 2015 walipoanzisha uhusiano wao wa kimapenzi kimya kimya.

 

Tazama mahojiano hayo hapa chini: