Nabii maarufu wa Zimbabwe aanzisha shule ya kuwafunza watu jinsi ya kufanya miujiza

Nabii alitangaza kwamba mafunzo hayo yataanza katika kipindi cha siku 7 zijazo na kuwataka watu wanaotaka kujiingiza katika ulimwengu wa kutenda miujiza kujisajili, kwani nafasi zinachukuliwa kwa haraka mno.

Muhtasari

•Nabii huyo ni mshirika wa karibu wa rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.

UBERT ANGEL
UBERT ANGEL
Image: FACEBOOK

Ubert Angel, mchungaji maarufu kutoka nchini Zimbabwe amegonga vichwa vya habari baada ya kutangaza kwamba ameanzisha shule ya kutoa mafunzo jinsi ya kutenda miujiza.

Angel, ambaye ni mshirika wa karibu wa rais wa taifa hilo Emmerson Mnangagwa alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwamba mafunzo hayo yataanza katika kipindi cha siku 7 zijazo na kuwataka watu wanaotaka kujiingiza katika ulimwengu wa kutenda miujiza kujisajili, kwani nafasi zinachukuliwa kwa haraka mno.

Kupitia instastory yake, Angel alipakia link ya kuelekeza mtu kwenye tovuti ya kujisajili na tulipoifuata, ilikuwa inatoa maelezo kuhusu jinsi mtu anaweza kujisajili na mengine mengi.

“Jisajili sasa na Ujifunze jinsi ya kufanya ishara miujiza na maajabu, mtandaoni, moja kwa moja kutoka kwa Nabii Uebert Angel. Nafasi zinajaa haraka,” chapisho kwenye Facebook yake lilisoma.

“Je, Uko Tayari Kuanza Safari Isiyo ya Kawaida ya Imani na Uwezeshaji? Shule ya Sayansi na Maajabu Sasa Imefunguliwa Kwa Usajili, Inaalika Nafsi Zenye Hamu Kutoka Kote Ulimwenguni Kugundua Sanaa ya Kufanya Miujiza. Iwe Wewe ni Kiongozi wa Kiroho Unayetafuta Kukuza Uwezo Wako wa Kiungu au Mtu Bila Kanisa Anayetafuta Muunganisho wa Kina na Miujiza, Mpango Huu Umeundwa Kwa Ajili Yako,” tangazo kwenye tovuti hiyo lilisoma.

Ubert Angel anaiita shule hiyo Shule ya Ishara na Miujiza.

Hata hivyo, hatukuweza kubaini kwa mara moja kiasi cha fedha anachotoza kama ada ya mafunzo hayo.