Rayvanny apagawa kukutana na shabiki wa filamu za Steven Kanumba Afrika Kusini

Kilichomshangaza Rayvanny ni kwanza shabiki mwenyewe ni raia wa Afrika Kusini ambapo hawaongei Kiswahili kabisa.

Muhtasari

• “Waigizaji wa Bongo, msiache kupambana sana, mtafika mbali,” aliwaasa waigizaji wa tasnia hiyo.

Rayvanny na Kanumba
Rayvanny na Kanumba
Image: Maktaba

Msanii Rayvanny ameonyesha bashasha na furaha yake baada ya kukutana na shabiki wa filamu za marehemu Steven Kanumba nchini Afrika Kusini.

Msanii huyo ambaye kaitka kipindi cha siku kama mbili hivi amekuwa akipakia video na picha akiwa anatumbuiza kwenye majukwaa mbalimbali Afrika Kusini alikutana na mrembo huyo na kushangaa kumfahamisha kwamba anapenda sana filamu za hayati nguli huyo wa kuigiza.

Kilichomshangaza Rayvanny ni kwanza shabiki mwenyewe ni raia wa Afrika Kusini ambapo hawaongei Kiswahili kabisa na pili ni kwamba ni binti mdogo anayezipenda filamu za Kanumba aliyefariki Zaidi ya miaka 11 iliyopita.

Alipakia video hiyo kwenye instastory yake na kusema kwamba shabiki huyo alimpunga na kuwataka waigizaji wa filamu za Kiswahili kutoziangusha juhudi za Kanumba kuiweka tasnia hiyo kidedea kiasi cha kuwavutia mpaka watu wasio na uelewa wa lugha ya Kiswahili.

“Kanumba alikuwa kitu kingine tofauti kabisa! Unaweza ukajiuliza ni miaka mingapi imepita tangu kufariki kwake, na huyu ni raia wa Afrika Kusini ambaye bado anazipenda na kuzifuatilia filamu zake. Bado Kanumba the Great anakumbukwa, mapenzi ya mahsabiki,” Rayvanny aliandika kwenye video hiyo akimsaili shabiki huyo.

Aidha, Rayvanny aliweza kubaini kutoka kwa shabiki huyo kwamba anaipenda sana filamu ya A Point of No Return, ambayo ni moja ya filamu za mwisho kutoka kwa gwiji huyo zilizoibuia kupendwa kabla na baada ya kifo chake cha ghafla.

“Waigizaji wa Bongo, msiache kupambana sana, mtafika mbali,” aliwaasa waigizaji wa tasnia hiyo ambayo inatajwa kuwa katika mmomonyoko wa kasi tangu kuondoka kwa Kanumba.

Kanumba alifariki dunia mwaka 2012.