“Mungu nijaalie niishi hadi miaka 70!” Video ya Chira akiomba maisha marefu kabla ya ajali

Brian Chira alifariki wiki mbili zilizopita akiwa na umri wa miaka 23 kufuatia ajali ya barabarani nyakati za alfajiri.

Muhtasari

• Mpaka kifo chake, kijana huyo alikuwa analelewa na nyanya yake baada ya mamake kufariki akiwa angali mdogo na babake akiwa hajulikani.

Mwanatiktok Brian Chira
Image: RADIO JAMBO

Sasa imebainika kwamba tiktoker mwendazake Brian Chira alikuwa na ndoto ya kuishi maisha marefu kabla ya umauti kumpata ghafla.

Katika video mpya ambayo imeibuliwa kwenye mtandao wa TikTok, Chira alionekana kwenye mahojiano na mwanablogu mmoja humu nchini na alisikika akisema kwamba ndoto yake kuu ni kuishi hadi kufikisha umri wa miaka 70.

“Kwa sasa nina miaka 22, na mpango wangu katika maisha ni kuishi hadi tuseme miaka 70, naomba Mungu anijaalie takwa langu,” Brian Chira anaonekana akisema kwa ukakamavu kwenye video hiyo.

Hata hivyo, ndoto hiyo yake ilipata kuzimwa ghafla baada ya kupata ajali kwa kugongwa na gari nyakati za alfajiri akisemekana kwamba alikuwa ametoka kuserereka kwenye tafrija ya klabu cha starehe usiku uliopita.

Kifo na shughuli nzima ya jinsi mazishi yake yalivyoendeshwa vimekuwa ni gumzo mitandaoni, baadhi wakiwapongeza jamii ya tiktok kwa kumpa heshima katika safari yake ya mwisho na wengine wakihisi kijana huyo alikuwa anaishi maisha yenye taabu kutokana na kukosa malezi mema.

Mpaka kifo chake, kijana huyo alikuwa analelewa na nyanya yake baada ya mamake kufariki akiwa angali mdogo na babake akiwa hajulikani.

Kijana huyo alijizolea umaarufu kutokana na video zenye utata ambazo alikuwa akizichapisha tiktok, aghalabu akiwa moja kwa moja na mashabiki wake.

Licha ya kusutwa na kuonekana kuchukiwa na wengi kipindi akiwa hai, alipendwa na wengi kipindi cha kifo chake, maelfu ya watu hususan vijana wakijitokeza nyumbani kwa nyanyake, Githunguri kushuhudia safari yake ya mwisho.