Vera Sidika akanusha kumpenda mtoto wake wa kiume zaidi kuliko wa bintiye

Kwa maelezo yake, Vera alisema kwamba wakati yuko nchini Kenya, muda mwingi akili yake huwa inafikiria tu malezi kwa wanao kiasi kwamba hadi anasahau kupiga picha.

Muhtasari

• “Vee niligundua unampenda sana Ice,” shabiki wake mmoja aliingia DM kumuuliza.

Vera Sidika na mwanawe.
Vera Sidika na mwanawe.
Image: Instagram

Mwanasosholaiti Vera Sidika amekanusha kuwa anawabagua wanawe katika kuwapa mapenzi ya mama.

Sidika aliichapisha picha akiwa amempakata kwa mbele mwanawe wa kiume, Ice Brown ambaye ni mdogo na hilo likawafanya baadhi ya mashabiki kuhisi kwamba ana mapenzi ya dhati kwake kuliko kwa kifungua mimba, Asia Brown.

Hata hivyo, Vera Sidika alikanusha vikali akisema kwamba yeye huwapenda wanawe kwa mapenzi sawa bila kuwabagua.

“Vee niligundua unampenda sana Ice,” shabiki wake mmoja aliingia DM kumuuliza.

“…na Asia hata Zaidi,” Vera alijibu na kuendeleza, “Jambo moja kunihusu mimi, nawapenda wanangu wote kwa mapenzi ya dhati. Kwa usawa kusema kweli.”

Mama huyo wa watoto wawili alijitetea kwa nini hakuposti picha akiwa na Asia.

Kwa maelezo yake, Vera alisema kwamba wakati yuko nchini Kenya, muda mwingi akili yake huwa inafikiria tu malezi kwa wanao kiasi kwamba hadi anasahau kupiga picha.

“Wakati niko nchini Kenya, mara nyingi huwa katika hali ya kutoa malezi kwa watoto kwa asilimia elfu moja. Huwa hata sifikirii kuhusu kupiga picha au hata kuchapisha mitandaoni,” Vera Sidika alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa msanii Brown Mauzo amekuwa akiwalea watoto hao baada ya kuachana rasmi mwezi Septemba mwaka jana.

Mauzo alitangaza kwamba baada ya kuishi pamoja kama mke na mume kwa takribani miaka 3 na kujaaliwa na watoto 2, ulifika wakati wote wakachokana na kila mmoja akaona ni bora kulibiringisha gurudumu la maisha yake pasi na uwepo wa mwenzake.

Vera tayari amefichua kumuingiza bintiye katika moja ya shule za kifahari jijini Nairobi.