Nimeambiwa mara nyingi siwezi lakini nawathibitishia naweza – KRG baada ya kukutana na Davido

KRG alisema kwamba anajiamini zaidi ya kauli za watu ambao wanashinda wakisema hawezi.

Muhtasari

• Licha ya muziki wake kutoshabikiwa pakubwa humu nchini, KRG amekuwa mmoja wa wasanii ambao wanaonekana kujuana sana na wasanii wakubwa kutoka nje ya nchi.

 

Davido akutana na KRG.
Davido akutana na KRG.
Image: INSTAGRAM

Msanii wa dancehall wa humu nchini KRG the Don amefichua kwamba yuko katika maandalizi ya kufanya kolabo ya kusisimua na msanii wa kimataifa kutoka Nigeria, Davido.

Akizungumza baada ya kukutana faraghani na msanii huyo ambaye alikuwa humu nchini wkendi ya Pasaka kwa ajili ya tamasha la Raha Fest, KRG alisema kwamba hiyo itakuwa mara nyingine tena kuonyesha ulimwengu na wale wanaombeza kwamba hawezi.

KRG alifichua kwamba kwa mara nyingi amekuwa akizisikia kauli za watu wakidai kwamba hawezi lakini mara kwa mara huwathibitishia kuwa anaweza, na hii ni safari nyingine ya kuonesha hilo.

Msanii huyo wa kujitapa sana alisema kwamba anajiamini kwa kiwango cha juu kupita kauli za wanaosema kwamba hana mashiko katika tasnia ya muziki wa humu nchini.

“Kama ungejua ni mara ngapi nimeambiwa siwezi, Ili tu kuthibitisha kuwa ninaweza, ungeelewa kwa nini nina imani ndani yangu. #Bughaaa Msanii Wa president Tuko na #OBO aka #Davido soon tunapika kitu cha viungo kwa watu wangu 😉” KRG aliambatanisha kwenye picha wakiwa na Davido.

Licha ya muziki wake kutoshabikiwa pakubwa humu nchini, KRG amekuwa mmoja wa wasanii ambao wanaonekana kujuana sana na wasanii wakubwa kutoka nje ya nchi.

Msanii huyo, aghalabu huonekana katika sehemu ya faragha na karibia wasanii wote wakubwa kutoka nje ya nchi ambao wanatua nchini, jambo ambalo limefanya baadhi ya watu kumuita “msanii deepstate.”

Lakini je, kuna asilimia ngapi ya uwezekano wa KRG kufanya kolabo na Davido?