Mara ya kwanza kukutana na Brian Chira alinipeleka KFC akaninunulia kuku - King Tizian Savage

“Wakati huo nilikuwa sijawahi kanyaga KFC na Chira amenipeleka na kujinunulia kuku, kutoka hapo nafikiri hata mimi nikashikamana na nikataka kuwa rafiki yake, kwa sababu mimi sikuwa nimeona kuku ya KFC," alisema.

Muhtasari

• Baada ya kukutana, Chira alimuambia nia yake ilikuwa kufanya video na walifanya video hapo na baadae akamchukua kwenye mgahawa wa KFC na kumnunulia kuku.

TIZIAN NA CHIRA
TIZIAN NA CHIRA
Image: FACEBOOK

Tiktoker anayevuma kwa sasa nchini Kenya, King Tizian Savage amefunguka mara ya kwanza walipokutana na rafiki wake wa karibu ambaye sasa ni marehemu, Brian Chira.

Akizungumza kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio humu nchini, Tizian alisema kwamba Chira ndiye alimtafuta baada ya kuona picha na video zake mitandaoni akisifiwa jinsi alivyokuwa mtanashati.

Tizian, ambaye kabla ya umaarufu wa tiktok alikuwa anafanya kazi ya kuendesha bodaboda jijini Nakuru anakumbuka kwamba Chira alimfuata mpaka kwenye steji alikokuwa akifanyia kazi, kwani alikuwa ni mtu maarufu sana kwa jina ‘cute nduthi guy’.

Baada ya kukutana, Chira alimuambia nia yake ilikuwa kufanya video na walifanya video hapo na baadae akamchukua kwenye mgahawa wa KFC na kumnunulia kuku.

“Mara ya kwanza tulikutana alikuwa anatetemeka, sijui alikuwa ananiogopa ama nini, akaniambia amekuja tukuwe marafiki tutengeneze content. Hiyo video hata iko kwa akaunti yake. Tukajuana na kutoka hapo akanipeleka hadi KFC na kuninunulia kuku.”

“Wakati huo nilikuwa sijawahi kanyaga KFC na Chira amenipeleka na kujinunulia kuku, kutoka hapo nafikiri hata mimi nikashikamana na nikataka kuwa rafiki yake, kwa sababu mimi sikuwa nimeona kuku ya KFC maishani mwangu, na hapa kuna mtu amekuja siku moja mmefanya video anakununulia, nilikuwa na furaha sana,” Tizian alikumbuka.

Baada ya hapo, Tizian alisema alifikiria imeisha hivyo lakini Chira akawa anampigia simu mara kwa mara anapokuwa mjini Nakuru na ikawa ni jambo la kawaida kukutana na kufanya video.

King Tizian alisema kwamba kutokana na Chira, alipata kujikusanyia umaarufu na mashabiki wengi naye akashikilia hapo na kuanza kujifanyia video zake.

Hata hivyo, Tizian alisema kwamba katika safari yake kuelekea kwa umaarufu TikTok, haswa mzizi ukitokea kwa Chira, alikutana na watu wengi ambao walianza kumchukulia kwamba ni mwanachama wa LGBTQ kutokana na jinsi Chira alikuwa anajibeba na kujikubali kuwa katika mreno huo.

Lakini alisisitiza kwamba yeye hayuko katika mrengo huo, huku akisema Chira alikuwa rafiki wake aliyemsaidia kujizolea jukwaa lake huru tiktok.