Otile Brown atangaza kuachilia wimbo wake wa injili wiki chache baada ya kuachia albamu

Akizungumza kuhusu himizo nyuma ya utunzi wa huo wimbo kwa jina ‘Hafanani’, Otile alisema kwamba ameimba juu ya vitu vingi lakini safari hii angependa kuimba juu ya Mungu.

Muhtasari

•  Katika wimbo huo kwa sehemu, msanii huyo anasikika akiguguna maneno kwamba hata kwenye ajali wala kifo haogopi wakati anajua kwamba Mungu wake yuko karibu naye kila wakati.

• Ujio wa wimbo huo unakuja wiki chache baada ya kuachia albamu yake yenye ngoma 15.

OTILE BROWN
OTILE BROWN
Image: Instagram

Siku chache baada ya kufokewa vikali na mashabiki katika tamasha la Raha Fest, msanii Otile Brown ametangaza kuachilia wimbo wake wa kwanza wa injili.

Kupitia Instagram yake, Otile Brown alipakia klipu aliimba wmbo huo na kuandika kwamba ni wimbo wake wa kwanza wa injili na ambao utatoka Kesho Ijumaa ya Aprili 5.

Akizungumza kuhusu himizo nyuma ya utunzi wa huo wimbo kwa jina ‘Hafanani’, Otile alisema kwamba ameimba juu ya vitu vingi lakini safari hii angependa kuimba juu ya Mungu.

“#Hafanani inashuka kesho... wimbo wa kwanza wa injili. Ngoja nimwimbie Bwana, niliimba mambo mengi lakini sikumwimbia kamwe 😔 mshuhudie kwa sauti yangu kesho,” Otile Brown alisema.

 Katika wimbo huo kwa sehemu, msanii huyo anasikika akiguguna maneno kwamba hata kwenye ajali wala kifo haogopi wakati anajua kwamba Mungu wake yuko karibu naye kila wakati.

Haya hapa ni baadhi ya maneno kwenye mishororo yake;

“Nimeshindikana, tena siogopi hata kwa ajali, ilmradi uko nami, niko sambamba, siogopi hata kwa ajali maana Mungu wangu mimi hafanani, yeye hafanani na binadamu…”

Ujio wa wimbo huo unakuja wiki chache baada ya kuachia albamu yake yenye ngoma 15 ikiwemo ‘One Call’ ambayo iliibuka kuwa pendwa kwa baadhi ya Wakenya haswa kutokana na kifo cha tiktoker Brian Chira.