Watarudi? Gidi Gidi azungumzia uhusiano wake wa sasa na Maji Maji, kurudi kwenye muziki

Gidi pia alizungumza kuhusu wao kufanya shoo moja ya mwisho kwa mashabiki wao, kusherehekea kazi zao za muziki.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo aliweka wazi kuwa wao bado ni marafiki wa dhati.

•Alisema siku hizi yeye na Maji Maji wanajishughulisha na mambo mengi yanayoweza kufanya iwe ngumu kwa wao kurudi kwenye muziki.

Maji Maji na Gidi
Image: HISANI

Mtangazaji wa Radio Jambo, na ambaye ni mwanamuziki wa zamani Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi amefunguka kuhusu uhusiano wake wa sasa na aliyekuwa mwenzake katika kundi la muziki la Gidi Gidi Maji Maji, Julius Owino almaarufu Maji Maji.

Katika mahojiano na KTN Home, mtangazaji huyo wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo aliweka wazi kuwa wao bado ni marafiki wa dhati.

Alifichua kuwa bado huwa wanakutana mara kwa mara, wanajuliana hali na kupata kubadilishana mawazo na kumbukumbu walizounda pamoja.

“Sisi ni marafiki wazuri. Sisi bado ni marafiki wazuri. Wakati mwingine tunakutana, wiki mbili zilizopita tulikuwa naye hapa,” Gidi alisema.

Aliongeza, "Tunashiriki mawazo, tunashiriki kumbukumbu zetu. Wakati mwingine tunakuwa na shinikizo la kurudi studio, lakini nguvu ya kuimba katika umri wetu haipo.

Tena aina ya muziki tuliofanya haidumu kwa muda mrefu. Ni muziki wa msimu, baada ya muda fulani unaenda.”

Mtangazaji huyo mahiri alibainisha kuwa siku hizi yeye na Maji Maji wanajishughulisha na mambo mengi ambayo yanaweza kufanya iwe ngumu kwa wao kurudi kwenye muziki.

Hata hivyo alidokeza kuwa hivi karibuni huenda wakafanya shoo moja kubwa ya mwisho kwa mashabiki wao kusherehekea maisha yao ya muziki yenye mafanikio.

"Tumekuwa tukifikiria kufanya shoo. Hivi karibuni tunapopata wakati au kuamua, au tupate shinikizo kutoka kwa mashabiki, tunaweza kufanya hivyo. Tunaweza kufanya shoo kwa mara ya mwisho,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Gidi pia alifunguka kuhusu wimbo wao maarufu ‘Unbwogable’ ambao waliimba zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Wimbo huo ulihusishwa sana na siasa, jambo ambalo mtangazaji huyo sasa amezungumzia ili kuweka mambo wazi.

"Unbwogable ilifanywa mwaka wa 2002, wakati wa uchaguzi wa 2002. Watu wengi wanauhusisha na uchaguzi wa wakati huo, ingawa kwetu haukuwa kuhusu uchaguzi," Gidi alisema.

Mwimbaji huyo wa zamani alifichua kuwa masaibu mengi ya maisha yalimsukuma yeye na Maji Maji kufanya wimbo huo ambao ulivuma sana Afrika nzima.

Alisema wakati huo alikuwa katika chuo kikuu kwa sasa na yeye na Maji Maji walikuwa hawajafanikiwa kutengeneza pesa licha ya bidii yao katika muziki.

“Nilikuwa katika chuo kikuu cha KCA. Maji Maji alikuja na kuniuliza “tutafanyaje sasa? Tumetoka tu kutengeneza albamu na bado hatupati pesa”.

Mimi nilikuwa nimeamua kurudi chuo na kuendelea na elimu yangu, kwa kweli nilikuwa tayari nimekata tamaa na kusema sitaki tena kufanya muziki.

Lakini Maji Maji alikuwa akiniambia ‘tufanye tu’. Kisha nikamwambia Maji, nadhani tuko Unbwogable. Mimi ni unbwogable. ilikuwa zaidi kujipa motisha,” alisema.

Bwogo ni neno la Kijaluo lenye maana ya ‘kutisha’, kwa hiyo ‘Unbwogable’ ilikusudiwa kumaanisha ‘huwezi kunitisha’