Shoga Jude Magambo maarufu kama Manzi wa Meru hatmaye ametimiza nadhiri yake ya kuendelea kumkumbuka aliyekuwa rafiki yake, marehemu Brian Chira milele kwa kuchora tattoo ya picha yake kwenye mgongo wake.
Katika video ambayo imekuwa ikienezwa mitandaoni, Magambo ambaye amekiri wazi wazi kuwa shoga alionekana akichorwa tattoo yenye picha maarufu ya Chira, picha sawia na ile ambayo kwa sasa anaitumia kama utambulisho wake kwenye ukurasa wa Instagram.
Magambo ambaye katika mahojiano na Radio Jambo wiki moja iliyopita alikiri kuwa rafiki wa karibu na Brian Chira alisema kwamba kifo chake kilikuwa ni pigo kwake na kwamba tayari anahisi kuna pengo kubwa lililobaki kwenye maisha yake kwa kuondokewa na Chira.
Hata hivyo, Magambo alikanusha kutoka kimapenzi na Chira, akisema kwamba ukaribu wao ulikuwa wa kirafiki tu.
“Hapana, sikuchumbiana naye. Ingawa, alikuwa mguso sana haswa wakati amelewa. Lakini hatukuwahi kuwa na mazungumzo hayo ya kuchumbiana,” Jude Magambo alimwambia mtangazaji Massawe Japanni.
“Nimem’miss sana Chira. Na nilikuwa nikishiriki naye mambo mengi. Wakati fulani, alikuwa kama ndugu yangu. Wakati ambapo naskia ako mbali, nilikuwa naskia kuna kitu kisicho sawa. Haikuwa inaisha hadi wiki moja kama sijamuaona, ama siku tatu,” aliongeza.
Chira alifariki mwezi mmoja uliopita kutokana na ajali ya barabarani majira ya alfajiri.