Mchungaji Lucy Natasha ametoa vidokezo muhimu kwako wewe uliyeko sokoni kutafuta mpenzi wa kuoa au kuolewa naye.
Kupitia mazungumzo kwenye chaneli ya YouTube ya Obinna, Lucy Natasha alisema kwamba kwa upande wa wanawake, mrembo yeyote anayeomba pesa katika mapenzi huyo hajafuata ndoa bali msaada.
“Aina ya kwanza ya mwanamke ambaye mwanamume yeyote anayetafuta mke hafai kumuoa, ni yule anayekupenda kwa sababu ya pesa. Kwa sababu katika kizazi cha sasa, wanawake wengi hawatafuti mapenzi, wanatafuta msaada, ambapo ni kizazi kibaya sana,” Natasha alianza kushauri.
“Kwa hiyo hawa hawako kwako kwa sababu ya moyo bali kwa sababu ya mkono, hawa huja kimakusudi kwa sababu ya kile ambacho watapata kifedha kutokana na uhusiano,” aliongeza.
Hata hivyo, mchungaji huyo alisema kwamba si vibaya kwa mtu kumpa pesa umpendaye lakini tatizo moja tu analo kwa wanaojificha ndani ya pesa kwa lengo la kupata pesa ni kwamba wengi wanataka kupokezwa bila wao kutoa.
“Kama mwanamke wakati unaolewa, kitu pekee ambacho unaleta mezani kisiwe ni cheti chako cha kuzaliwa. Ukiolewa kama mwanamke pia sharti uwe na uwezo wa kuleta mezani vitu kama title deed, logbook, biashara, kampuni. Ni lazima tuwe na kizazi cha wanawake ambao kazi yao sio tu kuchora eyebrows, tuwe na wanawake wanaoweza kuchora eyebrows na mipango ya kibiashara pia,” alisema.
Kwa upande wa wanawake walioko kwenye saka saka za mpenzi, Natasha aliwashauri kuangalia kwa mtu aliyeokoka.
“Kama hajaokoka huyo sio mwanamume wako, hata kama ni mrefu, mweusi na mtanashati, kama hajaokoka muondoe kwenye orodha ya wanaume unaotaka kuolewa nao. Unajua unahitaji mwanamume ambaye atakuwa kama nguzo yako ya Imani, ambaye Imani zetu zinawiana,” Natasha alisema.