Aliyekuwa mgombea wa ubunge Kamkunji, Alinur Mohamed ambaye ni shabiki kindakindaki wa Arsenal amefichua kwamba ameelekea nchini Ujerumani kushuhudia mubashara mtanange wa robo fainali ya ligi ya mabingwa baina ya Bayern Munich na Arsenal.
Mtanange huo mkali utaamua nani atakayejiunga na Borrusia Dortmund na PSG kwenye nusu fainali, ikiwa raundi ya kwanza mechi iliisha sare ya mabao 2-2 ugani Emirates nchini Uingereza.
Alinur alisema kwamba atakuwa Mkenya na Mwafrika wa kwanza kuwahi kushuhudia mechi ya moja kwa moja ya robo fainali ya ligi ya mabingwa inayohusisha timu ya Arsenal.
“Nimeondoka nchini kwenda kujiunga na Arsenal nchini Ujerumani katika uwanja wa Allianz Arena. Nitakuwa Mkenya wa kwanza na Mwafrika wa kwanza kuitazama Arsenal ikicheza moja kwa moja kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE ROBO FAINALI,” Alinur alisema huku akionesha picha akiwa kwenye ndege.
Akizungumza kama shabiki wa Arsenal, Alinur alisema kuwa ana matumaini ya Zaidi ya asilimia 100 kuwa timu yake itafuzu kuingia nusu fainali kwa kuichabanga mwenyeji Bayern Munich.
Pia alisema kuwa ana mpango wa kuialika timu nzima ya Arsenal kuja Kenya ili kuwapa motisha vijana wapenda soka.
“Nina uhakika 101% Arsenal itaiondoa Bayern Munich nje ya UCL. Pia nitawaalika Arsenal nchini Kenya na kuwakaribisha timu nzima wanapowashauri vijana wetu,” alisema.
Wengi wanahisi kwamba Arsenal ina matumaini finyu ya kufuzu nusu fainali baada ya kuruhusu sare ya 2-2 wiki jana wakiwa nyumbani Emirates.
Katika mechi hiyo, Bayern walicheza bila hata shabiki mmoja uwanjani kutokana na adhabu ya UEFA kwa mashabiki wao kwa kutupa fataki uwanjani katika mechi ya awali dhidi ya Lazio kufuzu robo fainali.