“Naamini Mungu ndio mwanzo anaanza na mimi!” – Nadia Mukami kwenye picha yake ya utotoni

Nadia Mukami ni mmoja wa wasanii wa kike humu nchini wanaofanya vizuri kwenye taaluma ya muziki na mwaka jana alishinda tuzo ya AFRIMMA kitengo cha msanii bora wa kike ukanda wa Afrika Mashariki.

Muhtasari

• Mama huyo wa mtoto mmoja na msanii Arrow Bwoy alipakia moja ya picha maarufu kutoka utotoni mwake akiwa peku na kuilinganisha na picha za baada ya mafanikio yake.

NADIA MUKAMI
NADIA MUKAMI
Image: Instagram

Malkia wa muziki wa kizazi kipya kutoka humu nchini Nadia Mukami amewarudisha mashabiki wake kwenye kumbukumbu za siku za utotoni mwake, kwa kupakia picha zake.

Mama huyo wa mtoto mmoja na msanii Arrow Bwoy alipakia moja ya picha maarufu kutoka utotoni mwake akiwa peku na kuilinganisha na picha za baada ya mafanikio yake.

Mukami alisema kwamba kurudisha kumbukumbu nyuma na kutafakari maisha yake ya sasa, analazimika kuamini kwamba kweli bado Mungu hajamalizana na yeye na ndio mwanzo anaanza kulifungua kapu lake la mafanikio.

“Bilionea wa siku zijazo. Eti huyu ni Nadia Mukami, Mungu yupo. Hakuna hali itakayodumu milele na Mungu huwa anakuja nyakati ambazo humtarajii kabisa. Naamini Mungu ndio mwanzo anaanza na mimi. Nimemtumainia tangu utotoni na hajawahi niangusha,” Nadia Mukami alisema.

Mukami alikumbuka wanafunzi wenzake shuleni akisema kwamba wengi wao sasa hivi ukiwakuta na uwaulize kumhusu, wengi watakuambia kuwa hawangetarajia msanii huyo msanii wa pop, kwani alikuwa ni mpenda vitabu sana.

“Alumnis wa Mount Laverna 2013 wanaeza kukwambia kwa watu hawangekuwa PopStars pengine kwa sababu naongoza orodha sababu mimi nilikuwa mpenda vitabu sana ila Mungu huyu fundi,’’ Mukami aliongeza huku akiwataka mashabiki wake kutumia maisha yake kuwahimiza wengine.

Nadia Mukami ni mmoja wa wasanii wa kike humu nchini wanaofanya vizuri kwenye taaluma ya muziki na mwaka jana alishinda tuzo ya AFRIMMA kitengo cha msanii bora wa kike ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika kitengo hicho, alikuwa anamenyana na wakali kutoka Tanzania, Zuchu na Nandy.