(Video) Familia ya Ex wa Manzi wa Kibera yaeleza sababu za kutaka azikwe makaburini Lang’ata

“Shamba lenye liko nyumbani sehemu ambayo anaweza akazikwa ambayo iko wazi ni kidogo sababu sehemu nyingine kubwa watu wamejenga nyumba." bintiye marehemu alieleza.

Muhtasari

• Hata hivyo, mjukuu wake alieleza kwamba kwa sasa hakuna hatua zozote zimepigwa katika maandalizi ya maziko ya babu yake.

Manzi wa Kibera na mchumba wake wa miaka 66
Image: INSTAGRAM// MANZI WA KIBERA

Huku maandalizi ya maziko ya mzee Nzuki mwenye umri wa miaka 67, aliyekuwa mpenzi wa mwanasosholaiti Manzi wa Kibera yakiendelea, familia yake sasa imejitokeza na kueleza sababu za kutaka azikwe katika makaburi ya Lang’ata.

Wengi walikuwa wanafikiria mwili wa mzee huyo aliyeaga dunia wikendi jana utasafirishwa hadi nyumbani kwake Ukambani lakini familia yake ikiongozwa na wanawe wawili na mjukuu wamejitokeza na kueleza sababu ambazo huenda zitafanya mazishi yake kufanyika makaburini Lang’ata.

Wakizungumza na waandishi wa habari za burudani baada ya Manzi wa Kibera kurejea Nairobi kutoka Mombasa na kukutana na wanafamilia hao, walieleza mipango yote ya mazishi huku wakiomba msaada wa kufanikisha safari ya mwisho duniani ya mzee Nzuki.

Bintiye marehemu alidokeza kwamba nyumbani kwao Ukambani kuna kesi ya mzozo wa shamba ambako walitarajia kumzika mzee huyo ni hivyo kuona ni heri azikwe Lang’ata ili kuepusha mzozo Zaidi.

“Shamba lenye liko nyumbani sehemu ambayo anaweza akazikwa ambayo iko wazi ni kidogo sababu sehemu nyingine kubwa watu wamejenga nyumba. Na sehemu nyingine kubwa ambapo angezikwa kwa sasa iko na kesi ya watu wa familia na wengine. Sasa hicho ndicho kizingiti ambacho kinaweza zuia asipelekwe nyumbani,” bintiye alieleza.

Aidha, binti huyo alieleza kwamba amefanya mazungumzo na watu wa nyumbani kwao akiwemo dadake Nzuki ambaye ni shangazi yake na wamekubaliana kuwa wanataka azikwe makaburini.

“Nimeongea na watu nyumbani kama dadake ambaye ni shangazi yangu, na wakoi wengine, tukakaa tukaona sababu tunaweza kumpeleka nyumbani na huo mzozo ambao uko nyumbani ulete mambo mengi, tukaona tumpeleke tu pale Lang’ata [Makaburini]. Sababu hapo tunaweza msindikiza tu na kumpumzisha kuliko tuende kule nyumbani tupeleke mambo mengine,” binti huyo aliongeza.

Hata hivyo, mjukuu wake alieleza kwamba kwa sasa hakuna hatua zozote zimepigwa katika maandalizi ya maziko ya babu yake, akisema kwamba bado watu wengine wa nje wanasubiria familia iamue kabla ya kujiunga nao kutoa misaada mingine hitajika.