“Iko shida!” Burale atoa maoni yake kuhusu wanaume kuchukua jina la mama kama jina la ukoo

Kwa maelezo yake, mtoto wa kiume haswa hujitambua yeye ni nani katika jamii kupitia kwa babake, na kumuita kwa jina la mama ni sawa na kumuachia maswali mengi yasiyo na majibu.

Muhtasari

• Burale kupitia ukurasa wake wa Facebook, alitoa maoni yake akisema mwanamume kuitwa kwa jina la ukoo la mama yake ni shida kubwa ambalo ipo kwenye meko inachemka.

• CEO wa MCSK Ezekiel Mutua katika upande wa kutoa maoni alionekana kumuunga mkono akisema kwamba mwanamume kamili hawezi kubali kuitwa kwa jina la mama.

Robert Burale
Robert Burale

Kwa muda mrefu hasa mitandaoni nchini Kenya, suala la watoto wa kiume kuitwa kwa jina la kina mama zao kama jina la ukoo limekuwa ni suala nyeti ambalo hakuna mwenye ujasiri kamili wa kulielezea.

Aghalabu, baadhi ya wanaume haswa kutoka upande wa uliokuwa mkoa wa Kati nchini Kenya huchukua majina ya kina mama zao kama jina la ukoo.

Hili, haswa huelezwa kwamba ni hatua inayochukuliwa na kina mama ambao huwa wamepata watoto na kukataliwa na baba zao, au kina baba kuingia mitini kwa kutoroka majukumu ya malezi.

Hata hivyo, mshauri wa kimaisha ambaye pia anajiongeza kama mchungaji, Robert Burale kwa ukakamavu wake ameamua kulikabili suala hilo ana kwa ana.

Kwa mujibu wa Burale, anahisi si sawa kabisa kwa mtoto wa kiume kuchukua jina la mama na kuifanya lake la ukoo, haswa hadi pale anapokuwa mtu mzima wa kujitegemea.

Burale kupitia ukurasa wake wa Facebook, alitoa maoni yake akisema mwanamume kuitwa kwa jina la ukoo la mama yake ni shida kubwa ambalo ipo kwenye meko inachemka.

Mchungaji huyo anahisi kwamba, japo ni suala nyeti, lakini linastahili kuzungumziwa hadharani na kudai hilo linaashiria mtoto wa kiume huenda akakumbwa na matatizo ya kujitambua yeye ni nani.

Kwa maelezo yake, mtoto wa kiume haswa hujitambua yeye ni nani katika jamii kupitia kwa babake, na kumuita kwa jina la mama ni sawa na kumuachia maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu uwepo na umuhimu wa baba katika maisha yake.

“Najua hii ni mada nyeti sana lakini naamini kuna tatizo wakati wanaume huchukua jina la mama yao kama jina la ukoo...MAONI YANGU YA UNYENYEKEVU (Naweza pia kuwa nimekosea). Mgogoro wa Utambulisho,” Burale alisema.

CEO wa MCSK Ezekiel Mutua katika upande wa kutoa maoni alionekana kumuunga mkono akisema kwamba mwanamume kamili hawezi kubali kuitwa kwa jina la mama.

Kulingana na Mutua, hata rais wa awamu ya 44 wa Marekani, Barack Obama angechukua jina la mamake lakini kwa kuwa yeye ni mwanamume kamili, aliamua kulichukua jina la babake licha ya kutokuwepo katika maisha yake ya utotoni.

“Haikuwa hivyo mwanzoni! Wanaume halisi hawafanyi hivyo haijalishi uhusiano na baba zao umekatishwa vipi. Obama angeweza kutumia jina la mama yake kwa sauti nyeupe, lakini yeye ni mwanamume halisi. Alishikilia mizizi ya mababu zake na alipoandika kitabu chake cha kwanza alikiita “Ndoto kutoka kwa Baba yangu” licha ya kwamba Mkenya huyo wa Kogelo alikuwa amewatelekeza. Obama halisi, alishikilia hadithi yake na akaibuka kutawala taifa lenye nguvu zaidi duniani! Kuna kitu kuhusu nasaba na ina mizizi katika ubaba, sio mama, muhimu kama mama!”

Maoni yako ni yepi kuhusu watoto wa kiume kuitwa kwa jina la ukoo la mama?