Diamond amtambulisha mrembo aliyemfanya kuandika ‘Nenda Kamwambie’ miaka 15 iliyopita

“Huyu ndiye Sarah, miaka 15 nyuma nilimuimbia huu wimbo si unajua kipindi hicho mbichi. Nilikuwa nikimuona namuona Beyonce nachanganyikiwa...na kile nilichokiimba humu ndani nilikiandika kwa sababu yake.”

Muhtasari

• Diamond aliwaomba wasaidizi wake kumpandisha mrembo huyo kwenye jukwaa kabla ya kumkumbatia na kuanza kuimba wimbo huo.

Diamond Platnumz
Diamond Platnumz
Image: screengrab

Wakati wa tamasha usiku wa Jumamosi, Diamond alifanya kufuru kwa kumtambulisha mrembo mmoja ambaye alidai ndiye chanzo cha yeye kuandika wimbo wa ‘Nenda Kamwambie’ ambao ulitoka takribani miaka 15 iliyopita.

Akiwa jukwaani, Diamond alirejesha kumbukumbu nyuma jinsi alivyoandika wimbo huo baada ya kumuona mrembo huyo kwenye ukumbi miongoni mwa mashabiki wake wengi waliofurika kushuhudia utumbuizaji wake.

Diamond aliwaomba wasaidizi wake kumpandisha mrembo huyo kwenye jukwaa kabla ya kumkumbatia na kuanza kuimba wimbo huo.

“Huu wimbo, niliimba maisha yangu ya ukweli. Unajua nilikuwa najaribu kuimba lakini kila mara nikijaribu nyimbo zinakuwa mbaya, sitoki. Kumbe nilikuwa kuna kiwango bado sikuwa nmekifikia, kulikuwa kuna maumivu ambayo ilikuwa lazima niyapate,” Diamond alianza kuhadithia.

“Na kuna dada mmoja nampenda sana, na leo nimemuona yumo humu ndani. Huyu dada anaitwa Sarah, huyu ndiye sababu ya mimi kuimba huu wimbo ‘Kamwambie’. Wakati huo alikuwa mtoto mdogo binti huyu,” Diamond aliongeza.

“Huyu ndiye Sarah, miaka 15 nyuma nilimuimbia huu wimbo si unajua kipindi hicho mbichi. Nilikuwa nikimuona namuona Beyonce nachanganyikiwa. Akanichamba matukio, ndio nikaenda kuandika huu wimbo, na kile nilichokiimba humu ndani nilikiandika kwa sababu yake,” Diamond alisema huku akithibitisha kwamba baadae walikutana na mrembo huyo wakayamaliza na kuwa marafiki.