Karen Nyamu awasikitikia waathirika wa mafuriko Mathare, aahidi kutoa msaada

Nyamu pia aliahidi kutoa misaada ya vyakula na bidhaa zingine za matumizi kwa wahanga wa mafuriko hayo kupitia kwa wakfu wake.

KAREN NYAMU
KAREN NYAMU
Image: instagram

Seneta mteule katika jimbo la Nairobi, Karen Nyamu amewasikitikia waathirika wa mafuriko katika mtaa duni wa Mathare, kaunti ya Nairobi.

Kupitia ukurasa wake, Nyamu alisikitika kwamba tayari eneo hilo liilokumbwa na mafuriko mabaya wiki jana limekwishapoteza watu 13 na mamia ya wengine kupoteza mali yao kutokana na mvua nyingi ambazo zinaendelea kunyesha tangia mwanzoni mwa mwezi huu.

“Moyo wangu unaumia kwa watu wa mathare ambao wameathiriwa zaidi na mafuriko katika jiji hilo na idadi ya vifo kuongezeka hadi 13,” Nyamu aliandika.

Seneta huyo alisikitika kwamba serikali haikuweza kuweka njia za kuzuia maafa Zaidi kutokana na mafuriko, mapema akisema kwamba ni wakati sasa serikali iweke mbele maslahi ya maisha ya mwananchi wa kawaida.

Nyamu pia aliahidi kutoa misaada ya vyakula na bidhaa zingine za matumizi kwa wahanga wa mafuriko hayo kupitia kwa wakfu wake.

“Kama nchi tunahitaji kuweka vipaumbele vya uwekezaji ili kurekebisha mifumo yetu ya mifereji ya maji sasa kuliko wakati mwingine wowote ili kututayarisha kwa mafuriko na kuzuia upotezaji huu wa maisha na kukatishwa kwa maisha yetu ya kila siku. Ni chungu kupita maneno kuwapoteza watu wetu kwa sababu ya hali ambayo tunaweza kuiona.”

“Timu yangu katika taasisi ya Karen Nyamu foundation itasambaza vyakula na vitu visivyo vya chakula kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko huko mathare na maeneo mengine ya Nairobi kama sehemu ya afua wakati mvua inaendelea,” Nyamu alisem.

Kufikia Jumapili, idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko nchini kote ilikuwa Zaidi ya 90 lakini Jumatatu asubuhi, taarifa mbaya ziliripotiwa na idadi hiyo kuongezeka kuzidi mika.

Hii ni baada ya boti kuzama katika Mto Tana usiku wa Jumapili huku pia makumi ya watu wakisombwa na maji katika eneo la Maai Mahiu baada ya bwana la Old Kijabe kuvunja kingo zake.