“Nakaribia kujuta!” Harmonize amjibu Diamond kwa kushinda akimkumbusha vile alimsaidia kimuziki

Kuhusu Diamond kumualika kwenye shoo yake, Harmonize alimjibu akisema kuwa yeye kwa sasa ni msanii mkubwa na Diamond hana uwezo wa kifedha kumlipa ili kutumbuiza kwenye moja ya shoo zake.

Muhtasari

• Diamond katika mahojiano mbalimbali haswa nje ya Afrika, amekuwa akiutaja moja kati ya michango yake mikubwa kwenye muziki wa Bongo ni kuwashika mkono na kuwainua Harmonize na Rayvanny.

Harmonize amjibu Diamond kisa kauli za kumsaidia kimuziki.
Harmonize amjibu Diamond kisa kauli za kumsaidia kimuziki.
Image: Facebook

Harmonize amevunja kimya chake baada ya Diamond kuendeleza mfululizo wa maneno yake ya kujitapa kuwa ametoa mchango mkubwa kwenye tasnia ya muziki kwa kuwasaidia baadhi ya wasanii kumuziki.

Katika mahojiano ya hivi juzi, Diamond alirejelea kauli hiyo tena akiwataja wasanii Harmonize, Richie Mavoko miongoni mwa wengine kama machipukizi ambao aliwashika mkono na kuwasaidia kimuziki.

Msanii huyo ambaye ni mkurugenzi wa lebo ya WCB Wasafi, si mara ya kwanza amekuwa akionesha fahari yake kwa wasanii kama Harmonize na Rayvanny ambao sasa wanajisimamia kimuziki.

Diamond katika mahojiano mbalimbali haswa nje ya Afrika, amekuwa akiutaja moja kati ya michango yake mikubwa kwenye muziki wa Bongo ni kuwashika mkono na kuwainua Harmonize na Rayvanny ambao kwa sasa nao wanamiliki lebo zao za kurekodi muziki.

Lakini kuradidi huku kwamba aliwasaidia kumeonekana kumfika kwenye koo Harmonize ambaye kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake na kumjibu aliyekuwa bosi wake akisema kuwa anakaribia kujuta kusaidiwa naye.

“Nilimtoa! Nilimtoa! Nilimtoa!.... ndio ni kweli na Ahsante, ila inachosha. Nakaribia kujuta!” Harmonize alisema akirejelea kauli za kurudia-rudia za Diamond jinsi alivyomsaidia kutoka na kutoboa kimuziki.

Harmonize
Harmonize

Diamond alisema kwamba anajivunia Harmonize na Rayvanny kama wanawe akisema kwamba baadae ndio atakuja kuanza kujivunia wajukuu ambao ni Ibra, msanii wa Harmonize na Macvoice msanii wa Rayvanny.

“Tajiri na mali zake, maskini na wanawe. Sasa mali mimi sina mzee Konde acha nijivunie nyie wanangu wa dhahabu. Nikitoka hapo nahamia sasa kwa wajukuu zangu Ibra na Macvoice. Kwenye miaka yangu 15 ya Sanaa nataka tufanye event moja ya ukoo mzima  na tusherehekee kidogo chenye Mungu alitubariki nacho,” Diamond alimuomba Harmonize.

Diamond
Diamond

Kuhusu Diamond kumualika kwenye shoo yake, Harmonize alimjibu akisema kuwa yeye kwa sasa ni msanii mkubwa na Diamond hana uwezo wa kifedha kumlipa ili kutumbuiza kwenye moja ya shoo zake.

“Tatizo maskini huyu hukumbuka wanawe akishakusanya mali zake. Hata hivyo, haiwezi kuja kutokea, hiyo miaka 15 maana milioni 600 huwezi kunilipa. Hutoweza! Sikia, unaweza kuwa mkubwa kwa kuwafanya wengine wadogo lakini pia unaweza kuwa mkubwa Zaidi kwa kuwafanya wengine wakubwa. Ulidai, nikakulipa, iwe mwisho, inachosha! Unachokinadi sasa hivi hustahili. Kka, huwezi kula keki yako tena uwe nayo mkononi,” Harmonize alifoka.

Ugomvi huu mpya umekuja kama shtukizi kwa mashabiki wa wasanii hao, ikizingatiwa kwamba ni hivi majuzi tu walionekana pamoja kwenye chakula cha futari ambapo waliweka makubaliano ya kusameheana na kudumisha urafiki kwa masilahi ya muziki wa Bongo Fleva.