Stevo Simple Boy avunja kimya baada ya mzozo wa muda kuhusu akaunti zake mitandaoni (video)

“Leo niko na mambo mpya manze, kuna mtu amekatalia akaunti zangu nimejaribu kufuatilia lakini imeshindikana. Kwa sasa hivi nimefungua akaunti mpya. Kwa hiyo naomba sapoti yenu." Stevo aliomba.

Muhtasari

• Kuhusu safari yake ya muziki kwenda mbele, Stevo alisisitiza kwamba kwa sasa hana uongozi akisema anajisimamia kimuziki mwenyewe.

STEVO SIMPLE BOY.
STEVO SIMPLE BOY.
Image: Instagram

Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, hatimaye msanii Stevo Simple Boy ametangaza kufungua akaunti za mitandao ya kijamii upya.

Rapa huyo wa ‘Freshi Barida’ kupitia akaunti mpya ya Instagram, alichapisha video akieleza kuwa amefikia uamuzi wa kuanza upya baada ya mzozo kuhusiana na akaunti zake za zamani kutozaa matunda yenye tija upande wake.

Msanii huyo alisisitiza kwamba kwa sasa yuko huru bila uongozi wowote akiwaomba mashabiki wake kumshika mkono kwa mara nyingine tena, kwa kumfuata kwenye akaunti mpya mitandaoni.

“Leo niko na mambo mpya manze, kuna mtu amekatalia akaunti zangu nimejaribu kufuatilia lakini imeshindikana. Kwa sasa hivi nimefungua akaunti mpya. Kwa hiyo naomba sapoti yenu. Twende pale Instagram, tiktok na YouTube, tufuate hizo akaunti ziwe na wafuasi wengi,” Stevo aliomba.

Kuhusu safari yake ya muziki kwenda mbele, Stevo alisisitiza kwamba kwa sasa hana uongozi akisema anajisimamia kimuziki mwenyewe.

“Kwa sasa hivi sina uongozi, najiongoza mwenyewe, na mashabiki wangu tafadhali mnisapoti mambo yawe vizuri, sio?” alimaliza.

Hatua ya Stevo kuanzisha akaunti mpya inakuja wiki mbili tu baada ya aliyekuwa meneja wake, Chingiboy Mstado kudai kwamba alikuwa amefikia uamuzi wa kuziachilia akaunti hizo kwa msanii huyo kupitia kwa mtu yeyote ambaye angejitokeza na kuonesha nia njema ya kumsaidia Stevo kuendeleza urithi wake kimuziki.

Awali, meneja huyo alikuwa ameshikilia msimamo wake wa kushikilia akaunti hizo hadi pale Stevo na watu wake watakapomfidia 150K alizodai kutumia kukomboa akaunti za Stevo kutoka kwa uongozi uliopita.

“Nafikiri ni muda mwafaka kwangu mimi kurudi chini ili nimsaidie ndugu yangu Stevo Simple Boy. Wakati mwingine hasira inaweza weka mtu pabaya. Nafikiri 150k si pesa ya maana sana kuliko taaluma ya kakangu Stevo. Ningeomba kama kuna mtu mkweli hapo nje mwenye anaweza kumsaidia Stevo, akuje nipatiane akaunti kwa Stevo ili wapige kazi kwa sababu watu wamemzunguka yule kijana watammaliza,” Chingiboy alisema katika taarifa yake wiki mbili zilizopita.