Aliyekuwa mchekeshaji ambaye sasa amegeukia katika ukuzaji maudhui kweny mitandao ya kijamii, Oga Obinna amewashangaza wengi baada ya kumtunuku mwanawe wa kiume simu aina ya iPhone 11 Pro kama zawadi ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Kijana huyo alikuwa anafikisha umri wa miaka 14.
Obinna alichapisha kionjo cha video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kusema kuwa video yote kwa ukamilifu ingepatikana kweney chaneli ya YouTube baadae Ijumaa.
Katika video hiyo, Obinna alipamba sherehe hiyo kwa madhari murua, huku akitumia nembo ya klabu ya Manchester United na chini yake kunakili umri mpya wa mwanawe, 14.
Wanawe wengine walikuwepo na baada ya kumwambia kugeuka na kuangalia upande mwingine, alichomoa simu mpya aina ya iPhone 11 pro kutoka kwenye kimkoba na kumkabidhi akimhakikishia kuwa hiyo ni mali yake kuanzia sasa kwenda mbele.
“Happy Birthday my G❤️❤️❤️ baba anakupenda mkuu. #theobinnaz #bigboss,” Obinna aliandika.
Obinna alisema kuwa kijana huyo ndiye alikuwa mwanawe wa kwanza na alimfunza mengi katika safari yake ya kwanza kabisa katika malezi.
“Mwanangu, mshindi wangu, moyo wangu. Kifungua mimba wa kwangu ameshatimiza umri wa miaka 14. Mtoto huyo alinifunza mengi kwa suala zima la malezi na uvumilivu. Ni mnyoovu, mtulifu na mwerevu,” Obinna alikumbuka.
Hatua ya kumpa mwanawe zawadi ya iPhone 11 Pro iliwasisimua mashabiki wake, wengine wakimhongera kwa jinsi ana ukaribu wa kipekee na wanawe licha ya kulelewa na kina mama tofauti.
Itakumbukwa ni hivi majuzi Obinna pia alifanikiwa kumnunulia mkuza maudhui mwenza, Dem wa FB simu aina ya iPhone 11 pro baada ya kukiri athari yake chanya katika ukuzaji maudhui kwenye chaneli yake ya Obinna Show Live.