Kanyari aeleza mbona hataki waumini wa kanisa lake kujiunga na mtandao wa TikTok (video)

" Wazimu wote duniani huwa wako TikTok. Mimi yale mambo ninasikua huko sijawahi yasikia kwingine tangu nizaliwe, lakini navumilia,” Kanyari aliwashauri waumini wa kanisa lake.

Muhtasari

• Katika moja ya klipu kutoka kwa mahubiri kwenye kanisa yake yaliyochapishwa kwenye ukurasa wa TikTok wa Shifu TV, Kanyari alionekana akiwashauri waumini wake dhidi ya mtandao huo.

Mchungaji wa kanisa la Salvation Healing Ministry, Victor Kanyari ametoa sababu za kuwataka waumini wa kanisa lake kutojiunga katika mtandao wa video fupi wa TikTok.

Katika moja ya klipu kutoka kwa mahubiri kwenye kanisa yake yaliyochapishwa kwenye ukurasa wa TikTok wa Shifu TV, Kanyari alionekana akiwashauri waumini wake dhidi ya mtandao huo.

Kwa mujibu wake ambaye ni mtumizi wa TikTok kwa wiki kadhaa sasa, alisema kuwa mtandao huo una maneno mengi, ambayo asingependa yawatoa waumini wake kwenye njia salama ya wokovu.

“TikTok iko na maneno, usiingie wewe,” Kanyari alianza kusema baina na vicheko vya mzaha. “Sitaki unione, wewe kaa huko kwa TV. Usiingie huko, huko kuna wazimu wa huko, wa Mathare wako huko. Wazimu wote duniani huwa wako TikTok. Mimi yale mambo ninasikua huko sijawahi yasikia kwingine tangu nizaliwe, lakini navumilia,” aliongeza.

Ushauri wa Kanyari kwa waumini wake unakuja wakati ambapo yeye karibia kila siku yuko kwenye mtandao huo akiwaomba watumizi wake kumfuata kwa wingi na hata kumtumia zawadi mbalimbali.

Hata hivyo, mchungaji huyo mwenye utata alijitetea akisema kwamba hakufuata pesa kwenye TikTok bali aliwafuata vijana ambao ndio asilimia kubwa ya watumizi wake, ili kuwahubiria, akidai wengi wamezingirwa na ibilisi.