Willy Paul aeleza sababu ya kuondoka katika injili na kujikita kwenye miziki ya kidunia

Hitmaker huyo wa ‘Kitanzi’ alifichua taarifa za ukakasi mwingi kwamba kama si kufanya uamuzi wa kujiondoa kwenye injili, pengine angeishia kujitia kitanzi au hata kuwa mwendawazimu.

WILLY PAUL.
WILLY PAUL.
Image: Instagram

Msanii anayezidi kutamba na albamu yake mpya ya Beyond Gifted, Willy Paul kwa mara ya kwanza amezungumzia jinsi alifanyiwa mazingira kuwa magumu katika tasnia ya injili mpaka kufikia uamuzi wa kujiondoa.

Akizungumza kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini, Pozee alisema kwamba kuna mambo mengi ambayo yalikuwa yanamtokea lakini asingependa kuzungumza wakati huo Zaidi tu ya kufanya uamuzi wa kubadilisha wimbi lake na kuelekea katika muziki wa sekula.

“Ni vitu vingi vilitokea, unajua wakati mwingine ukiwa unahisi hapa penye niko nisipotoka nitauliwa, ukiwa kwa hali kama hiyo inabidi ujiondoe katika hayo mazingira. Kuna mambo mengi yalikuwa yanatokea wakati nafanya injili huko. Sitaki kuanza kunyoosha vidole za lawama lakini wenyewe wanajua,” Pozee alisema.

Hitmaker huyo wa ‘Kitanzi’ alifichua taarifa za ukakasi mwingi kwamba kama si kufanya uamuzi wa kujiondoa kwenye injili, pengine angeishia kujitia kitanzi au hata kuwa mwendawazimu.

Anasema kwamba hajutii hata kidogo hatua yake ya kuondoka injili na kukumbatia sekula.

“Watu wenye nilikuwa nao wanajua chenye walinifanyia lakini ni venye sikutaka kuizungumzia, lakini ilinipasa kuendelea mbele, na mimi nikifanya hatua huwa sijutii, hivyo sijutii kuwa penye niko leo. Kama singefanya huo uamuzi mngesikia pengine huyo jamaa alijiua au alichizi, sijui niseme hayo mazingira yalikuwa ya kusimanga sana,” aliongeza.