Ilinivunja moyo!Jinsi sherehe ya siku ya kuzaliwa ilivyoathiri akili ya Kimani Mbugua,baba yake aeleza

Kufuatia hali hiyo, babake Mbugua alianza kuchunguza kilichompata mwanawe siku zilizopita.

Muhtasari
  • Mchekeshaji Obinna na wanaume wengine kadhaa nchini wameungana katika harakati za kumsaidia mwanahabari huyo wa zamani.
Kimani Mbugua
Kimani Mbugua
Image: HISANI

Aliyekuwa Mwanahabari wa Citizen TV Kimani Mbugua amekuwa akitoa matamshi  ya wasiwasi kwenye mitandao ya kijamii ambayo yamehusishwa na hali yake ya kiakili.

Mchekeshaji Obinna na wanaume wengine kadhaa nchini wameungana katika harakati za kumsaidia mwanahabari huyo wa zamani.

Obinna alikuwa na mazungumzo na babake Mbugua, ambaye alifichua kwamba yeye ndiye mwana pekee na mzaliwa wa kwanza kati ya dada watatu.

Babake Mbugua aliendelea kueleza jinsi maisha ya Kimani Mbugua yalivyobadilika baada ya siku yake ya kuzaliwa mwaka wa 2020.

Alifichua kuwa maisha ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 yalikuwa sawa, alipata A katika shule ya upili na akachagua uandishi wa habari badala ya udaktari kama familia yake ilivyotamani.

Baadaye alipata nafasi ya kazi katika Nation Media Group kabla ya kuenda Royal Media Services. Pia alikuwa akiwatunza wadogo zake.

Mambo hata hivyo yalichukua mwelekeo tofauti mnamo 2020 Februari.

“Nilikuwa Westlands ofisini, nikampigia simu, nina kampuni inayojishughulisha na masuala ya ushauri na ni mkurugenzi mwenzangu. Tulipokuwa kwenye chumba cha mikutano kwenye kikao, alisimama na kuniambia baba, kwa siku nne sijaisha ulevi. Nikashtuka na sisi ni SDA, pombe imetoka wapi? Aliposema hivyo, akaketi, akanipa red flag. Aliegesha gari kwa basement akaacha milango ikiwa imefunguliwa, na hakuwa amechelewa that gave me a very heavy signal,” babake Mbugua alikumbuka.

Siku hiyo hiyo usiku, babake Mbugua alipokea simu kutoka kwa mpenzi wake akisema kwamba alikuwa akiongea bila kukoma.

“Niligundua red flag nyingine akanifanya nisikilize anachozungumza na nikasikia mambo ambayo sikuweza kuelewa. Ilinitia wasiwasi hadi leo,” alikumbuka.

Siku iliyofuata, Kimani alipelekwa katika hospitali ya Avenue kwa nia ya kujua ni nini kilikuwa kibaya.

“Nilikuta mtoto wangu amefungwa kamba, hanijui, hanitambui na anaongea na kuongea. Ilikuwa machafuko. Ikanivunja moyo. Aliponiona aliniita majina yangu halisi, ‘Mbugua! yule mzee alisimulia.

Kufuatia hali hiyo, babake Mbugua alianza kuchunguza kilichompata mwanawe siku zilizopita.

"Alikuwa na sherehe ya kuzaliwa. Nikiwa nafanya uchunguzi wa wazazi, yule dada alichukua simu yake na kupitia picha zake za sherehe. Akaona pale anatapika anaanguka anapigwa anaambiwa maneno na kabla ya hapo, binti yangu alidai aliona dawa nyeupe inawekwa kwa glasi yake na anaambiwa kunywa, ile unga unga,” babake Mbugua alisema na kufichua kuwa kinywaji cha mwanawe kilikuwa na kokeini.