KRG amponda Kanyari baada ya video akipokea zawadi za kondomu kwenye mimbari kanisani

Kanyari alijiunga katika mtandao wa TikTok miezi michache iliyopita, na amekuwa akishiriki vipindi vya mubashara akifanya mambo ya ajabu na kutamka vitu vya kustaajabisha, katika kile ambacho anadai ni kueneza injili kwa vijana wa TikTok.

Muhtasari

• “Mungu yuko na Ukristo ni dini nzuri lakini walaghai wazembe hawajui ni lini kuacha utapeli wao wa kipumbavu,” aliongeza.

KRG
KRG
Image: Instagram

Msanii KRG the Don amekuwa wa hivi punde kutoa maoni yake kuhusu kile kinachoendelea humu nchini kumhusisha mchungaji Victor Kanyari na sarakasi zake kwenye jukwaa la TikTok.

Kanyari amekuwa gumzo kwa njia hasi siku chache baada ya tukio la ajabu kushuhudiwa katika kanisa lake ambapo tiktoker wa kike alimkabidhi zawadi za kondomu kwenye mimbari ya kanisa lake.

Kwa mujibu wa KRG, Kanyari amevuka mipaka katika kutumia Ukiristo vibaya kama njia ya kutafuta kiki.

KRG anahisi kwamba kumekuwa na ongezeko la wachungaji wa kustaajabisha ambao wameifanya dini ya Ukristo kuonekana kama mzaha, akisema kuwa Ukiristo sio mbaya bali ni wale ambao wamepewa kibali cha kuongoza kondoo wa Mungu wanaokosea.

“Baadhi ya wachungaji wa kustaajabisha wanaifanya dini ya Ukristo kuonekana kama mzaha wakati mwingine. Wakatae wahubiri wa kustaajabisha kama hawa makanisani tafadhali,” KRG alishauri.

“Mungu yuko na Ukristo ni dini nzuri lakini walaghai wazembe hawajui ni lini kuacha utapeli wao wa kipumbavu,” aliongeza.

Kauli za KRG zinazokisiwa kumlenga Pasta Kanyari zinakuja saa chache baada ya msanii mwenza, Nadia Mukami kumsuta vikali mchungaji huyo kwa kile alisema ni kufanyia mimbari mzaha.

Mukami anahisi kwamba ni wakati Kanyari akuwe na mipaka na aweze kutofautisha wakati wa kumtumikia Mungu kwenye mimbari kanisani na wakati wa kufanya kiki ili mambo yake yaende kwenye mitandao ya kijamii.

“Hiyo video ya Mchungaji Kanyari ni ya ukakasi, kuna mipaka ya mimbari, hii hali ya kufanya maudhui inastahili iwe na mipaka jamani. Ikiwa si kwa heshima ya kanisa na dini yetu, basi iwe ni kwa ajili ya kumcha Mungu. Mimbari haichezewi,” Mukami aliandika.

Jumapili, Kanyari alipokezwa zawadi za vifurishi vya kondomu, mafuta ya kujipaka na vitu vingine kanisani na mwanadada ambaye ni maarufu kwenye TikTok.

Kanyari alijiunga katika mtandao wa TikTok miezi michache iliyopita, na amekuwa akishiriki vipindi vya mubashara akifanya mambo ya ajabu na kutamka vitu vya kustaajabisha, katika kile ambacho anadai ni kueneza injili kwa vijana wa TikTok.