Robert Kiyosaki: Mwandishi wa ‘Rich Dad Poor Dad’ afichua kwa nini hakuwahi kuja Kenya awali

“Niko Nairobi, Kenya. Sijawahi kufika hapa kabla, ingawa nimekuwa nikija Afrika takriban mara moja kwa mwaka kwa takriban miaka 20" alisema Kiyosaki.

Robert Kiyosaki
Robert Kiyosaki
Image: Facebook

Robert Kiyosaki, mjasiriamali na mwandishi marufu wa vitabu vya mafunzo ya elimu ya kifehda, ‘Rich Dad Poor Dad’ hatimaye ametua nchini Kenya baada ya kughairi kufanya hivyo kwa Zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Kiyosaki kupitia ukurasa wake kwenye jukwaa la X alieleza furaha yake baada ya kufika Kenya kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya miaka 77.

Akizungumzia sababu ambazo zimekuwa zikimzuia kuingia Kenya kwa miaka 20 iliyopita licha ya kutembelea mataifa mbalimbali Afrika, Kiyosaki alisema kuwa ni kutokana na marufuku ya uwindaji iliyowekwa na serikali ya Kenya tangu enzi za miaka ya 60s.

Mwandishi huyo kutoka Marekani alisema kwamba hicho kilikuwa kizingiti kikubwa sana kwake, ikizingatiwa kwamba yeye ni mwindaji wa kiasili.

“Niko Nairobi, Kenya.  Sijawahi kufika hapa kabla, ingawa nimekuwa nikija Afrika takriban mara moja kwa mwaka kwa takriban miaka 20. Sababu ambayo sikuwahi kufika Kenya ni kwa sababu walitoka katika uwindaji haramu miaka ya 1960 na mimi ni mwindaji,” Kiyosaki alisema.

Hata hivyo kwa kurudisha kisengere nyuma, Kiyosaki alisema kwamba hatua ya serikali ya Kenya kupiga marufuku uwindaji haramu kipindi hicho inalipa kwa sasa kwani Kenya ni moja ya nchi nzuri kwa watalii wapenda wanyama, kama mke wake ambaye anapenda na kufuga wanyama.

“Nina furaha niko Kenya leo kwa sababu sasa ninaelewa jinsi viongozi wao walivyokuwa werevu, wakipiga marufuku watu kama mimi….mwindaji. Kenya ni bora kwa wapenzi wa wanyama kama mke wangu Kim ambaye huwalinda na kuwapenda wanyama wote.”

“Ulimwengu ni mkubwa wa kutosha kuwapa watu maoni yanayopingana, maoni yao wenyewe. Naipongeza Kenya kwa kuchukua msimamo kwa ajili ya Afrika na kuwalinda wanyama,” aliongeza.