Mchungaji Kanyari aomba radhi baada kuzawadiwa mipira ya kondomu kanisani

Alijitetea akisema kuwa hakufahamu kilichofungwa kwenye gazeti alilopewa akisema alishtuka.

Muhtasari

•Wakenya walimshtumu Kanyari, huku baadhi wakisema kuwa yeye si mtu wa Mungu wa kweli, hivyo kumlazimu kuomba msamaha hadharani.

•Kanyari alisema tukio kama hilo halitajirudia tena, akiongeza kuwa hakutaka kumfukuza Imani, akihofia waumini wake wangemshambulia.

Pastor Kanyari
Pastor Kanyari
Image: HISANI

Mchungaji Victor Kanyari aliwaomba radhi waumini wa kanisa lake na Wakenya kwa ujumla baada ya video zake akipewa zawadi ya kondomu na TikToker Faith Peters wakati wa ibada ya kanisa kusambaa mitandaoni.

Mchungaji Kanyari amejitokeza kuomba msamaha baada ya kukosolewa sana mtandaoni.

Mwanzilishi huyo wa Salvation Healing Ministry alichapisha video iliyoonyesha akiwaomba radhi Wakenya baada ya kukashifiwa kwa kutaniana na mwanamke aliyempa zawadi ya kondomu wakati wa ibada ya moja kwa moja kanisani.

Naomba radhi kwa kilichotokea Jumapili iliyopita,” alisema.

Mhubiri huyo mwenye utata alijitetea akisema kuwa hakufahamu kilichofungwa kwenye gazeti alilopewa akisema alishtuka.

"Mimi nimefanyia Mungu kazi miaka 30 na sijawahi ona kitu kama hio. Sijawai ona mtu analeta vitu kama hizo kanisani. Hakuna mtu afanyangi makosa, msichana alikosea na sikutaka kumpiga au kumtusi kwa sababu washirika wangempiga,” alisema.

Kanyari alidai kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwa binti huyo kufika kanisani kwake, na hakuwa ameokoka.

Mwanzilishi wa Salvation Healing Ministry alisema tukio kama hilo halitajirudia tena.

“Si kujua nini kilikua ndani ya gazeti na  Naomba msinisamehe kwa jambo lililotekea. Jambo kama hilo halitatokea tena.” Alisema.