“Matumaini ni kuomba mvua, imani ni kubeba mwavuli!” – MP Babu akiombewa na Rev Natasha

Ikumbukwe kumekuwepo na minong’ono ya chini kwa chini kwamba Babu Owino anajiandaa kuwania wadhfa wa ugavana katika jimbo la Nairobi japo mwenyewe hajatamka hivyo.

Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amewafurahisha wafuasi wake katika mitandao ya kijamii baada ya kuchapisha picha kutoka kwa mkutano wake na mchungaji wa kanisa la Empowerment Cristian Church, Lucy Natasha.

Katika picha hizo, Owino alionekana akifanyiwa maombi na Rev Natasha, na kuthibitisha mwenyewe kwa maelezo ya kuzisindikiza picha hizo kwamba alikuwa anapokezwa chakula cha kiroho na mtumishi wa Mungu.

Mbunge huyo alitoa mfano wa kinadharia kwamba kuwa na matumaini katika kuombea mvua kunaashiriwa na Imani ya kubeba mwavuli ukijua kwamba baada ya kuomba mvua, itanyesha hatimaye na utahitaji kujikinga dhidi ya mvua kwa mwavuli.

“Nilipokea lishe ya kiroho kutoka kwa Mchungaji Lucy Natasha. Matumaini ni kuombea mvua, lakini imani ni kuja na mwavuli,” Owino alisema.

Kwa upande wake, mchungaji Natasha alishukuru ufanisi wa mkutano wake na mbunge huyo akisema kwamba muda wote ni vyema kujihusisha na watu ambao wana tija kwa upande wake.

Natasha alifichua kwamba moja ya jambo ambalo walilizungumzia ni kuhusu mikutano ya injili inayoendeshwa na kanisa la ECC katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi.

“Jizungushe na watu chanya wanaozungumza juu ya maono, maoni na suluhisho. Dakika Za Ajabu Zamani Na Ndugu Yangu Mhe. @he.babuowino , Mbunge wa Jimbo la Embakasi Mashariki. Nilimweleza kuhusu programu zetu za mawasiliano ndani ya jiji na kuchunguza maeneo ya ushirikiano wa pande zote tunapogusa jumuiya zetu,” Rev Natasha alisema.

Ikumbukwe kumekuwepo na minong’ono ya chini kwa chini kwamba Babu Owino anajiandaa kuwania wadhfa wa ugavana katika jimbo la Nairobi japo mwenyewe hajatamka hivyo.

Babu ni moja kati ya wabunge wachanga kwenye bunge la kitaifa, akiwa katika muhula wake wa pili na mtetezi wa kudumu kwa sera za kinara wa ODM, Raila Odinga.