Mchekeshaji Makokha aomba msaada wa kifedha kufanikisha mazishi ya marehemu mkewe

Taarifa hizi zilifichuliwa na mwenyekiti wa kamati inayosimamia mipango ya mazishi ambaye pia ni muigizaji mwenza kwa muda mrefu Hiram Mungai Ngigi maarufu kama Ondiek Nyuka Kwota.

Makokha na marehemu mkewe
Makokha na marehemu mkewe

Mwigizaji wa ucheshi wa muda mrefu katika kipindi cha Vioja Mahakamani kwenye runinga ya KBC, Matayo Keya maarufu kama Alphonse Makokha ameomba msaada wa kifedha kufanikisha mazishi ya marehemu mkewe aliyefariki siku chache zilizopita.

Taarifa hizi zilifichuliwa na mwenyekiti wa kamati inayosimamia mipango ya mazishi ambaye pia ni muigizaji mwenza kwa muda mrefu Hiram Mungai Ngigi maarufu kama Ondiek Nyuka Kwota.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Nyuka Kwota alichapisha picha za Makokha na marehemu mkewe Purity Wambui wakiwa pamoja enzi za uhai wake na kusema kwamba marehemu aliacha bili ndefu ya hospitalini na familia hiyo inahitaji msaada wa mashabiki wake katika kumpa buriani ya maana.

“Tunakufikia wakati wa mahitaji. Mchekeshaji wetu kipenzi Matayo Msagani Keya, anayefahamika na wengi kwa jina la Makokha•Makacha "BabyFace" anakabiliwa na wakati mgumu. Mkewe mpendwa, Purity Wambui Msagani, ameaga dunia kwa masikitiko, na tunaomba usaidizi wako usaidie kulipia bili yake ya hospitali na kumpa send-off inayostahili.”

“Ikiwa ungependa kumuunga mkono Matayo katika kipindi hiki kigumu, tafadhali tuma michango yako kwa akaunti ifuatayo:Akaunti/Nambari ya Mpaka: 7870966. Jina la Akaunti: Shanice Njeri Msagani. Ukarimu na wema wako unathaminiwa sana,” Nyuka Kwota aliomba.

Siku mbili zilizopita, Nyuka Kwota alitaarifu umma kuhusu kifo cha mkewe Makokha kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, taarifa ambazo ziliwapata wengi kwa mshangao mkubwa.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua kwa undani chanzo cha kifo cha marehemu.